Mwandishi Wetu
Kiwanda cha kuchakata bidhaa za ngozi cha Karanga kinatarajiwa kuzalisha ajira 3000 katika fani mbalimbali nchini mara baada ya kukamilika ujenzi wa jengo la kuchakata bidhaa za ngozi lililo katika hatua za mwisho.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati akitoa majumuisho ya ziara yake katika kiwanda hicho alipotembelea kukagua na kuona maendeleo ya ujenzi huo tarehe 7 Januari, 2021 mkoani Arusha.
Waziri alieleza kuwa, kiwanda hicho hadi sasa kimeajiri wafanyakazi 283 kati 3000 ambapo mpaka mwezi Juni mwaka huu kinatarajia kuajiri wafanyakazi 1906 katika maeneo mbalimbali.
“Kiwanda hiki kinamanufaa kwa jamii kwakuwa kitachangia kutatua changamoto ya ajira kwa vijana wetu hivyo kamilisheni kwa wakati na uzingatie thamani ya fedha zilizowekezwa,”alisema Waziri Mhagama
Waziri aliwataka kuhakikisha ifikapo Juni, 2021 mradi huo unakamilika na kuukabidhi kulingana na makubaliano ya ujenzi huo.
Aidha kiwanda kinalenga kuwa na uzalishaji mkubwa utakao changia katika uchumi wa nchi na kupata faida ili fedha zilizowekezwa na wananchi zisitumike pasipo matokeo yaliyokusudiwa.
Waziri aliwataka kuhakikisha kiwanda kinakuwa endelevu na kuzalisha bidhaa zenye viwango ili kujihakikishia soko la uhakika.
“Hakikisheni mnatoa bidhaa zenye ubora na anzeni kutafuta masoko ili kuepuka changamoto ya soko la uhakika,”alisema
Naye Msimamizi wa Ujenzi wa kiwanda hicho Dkt. Miragi Katumbili aliahidi kuendelea kisimamia na kuhakikisha kiwanda kinakamilika kwa wakati ili kusaidia ajira hizo kwa vijana pamoja na kuahidi kuendelea kusimamia kwa ufanisi wa hali ya juu.
“Tunaahidi ujenzi utakamilika kwa wakati, kama uliyotupa miezi sita,na ifikapo mwezi Juni 2021 tutakuwa tumekabidhi mradi huu,”alisema Mhandishi Mitagi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa umma (PSSSF) Bw. Hosea Kashimba aliahidi kutekeleza maelekezo ya waziri ikiwemo kuendelea kutoa fedha za ujenzi huo kwa wakati.
Alieleza matarajio ni kukamilisha ujenzi kwa wakati na kufikia malengo ya kuzalisha bidhaa kwa wingi zenye kuchangia kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
“Kama wafadhili wa mradi huu,tutahakikisha tunatoa fedha na malighafi kwa wakati ili kutokwamisha ujenzi huu unaoendelea,”alisema Kashimba.
Alimwakikishia Waziri uwepo wa soko kubwa la viatu ndani na nje ya nchi ambapo hadi sasa kiwanda kimepokea mahitaji ya kutengeneza viatu 48000 na kueleza ni ishara nzuri kwa kiwanda hicho.