NEWS

2 Machi 2021

Agizo la ujenzi wa vyumba vya madarasa 2257 latekelezwa


 Na Atley Kuni, DODOMA
Serikali imetekeleza agizo la Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa lililozitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa ujenzi wa vyumba vya madarasa 2257 uwe umekamilika ifikapo Februari, 28, 2021.

Akitoa taarifa mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amesema, kukamilika kwa madarasa hayo kutaziwezesha halmashauri zote nchini kuwapokea wanafunzi 112,850.

Amesema kulingana na idadi hiyo ya wanafunzi kwa vyumba 2257 kila darasa litakuwa na uwezo wa kuwapokea wanafunzi 50.

“Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Serikali kwa ujumla, inawapongeza Wananchi, Wadau mbalimbali wa Elimu, na Watendaji wote wa Serikali walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika ujenzi wa vyumba vya madarasa hayo,” amesema Mhe. Jafo

Aidha, Waziri Jafo amesema jumla ya vyumba vya madarasa 1374 vinaendelea kukamilishwa na vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi, na wanafunzi wote 74,166 waliokuwa wamekosa nafasi ya kuanza kidato cha kwanza sasa wamepangiwa shule sawa na maelekezo ya serikali.

Pia Waziri Jafo amewataka viongozi wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kusimamia kwa karibu ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwakani.

“Mikoa na Halmashauri zote zinaelekezwa kuanza kufanya uchambuzi wa mahitaji ya vyumba vya madarasa kwa ajili ya darasa la awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2022, na wasisubiri maelekezo ya Serikali kuu,” amesisitiza Mhe. Jafo

Mwezi desemba mwaka 2020 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alifanya Mkutano na Wakuu wa Mikoa Tanzania Bara kujadili namna ya kuwapokea wanafunzi wa Kidato cha Kwanza Mwaka 2021 na kupitia kikao hicho aliwaagiza Wakuu wote wa Mikoa kuhakikisha wanafunzi wote wenye sifa za kujiunga na Kidato cha Kwanza ambao hawakupangiwa shule katika awamu ya kwanza wapate nafasi ifikapo tarehe 28, Februari, 2021.