NEWS

2 Machi 2021

Waziri Kalemani Aagiza Mtambo Wa Umeme Kidatu Kufanya Kazi Ndani Ya Siku 15


 Na Teresia Mhagama, Morogoro
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani, ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhakikisha kuwa, mtambo namba mbili wenye uwezo wa megawati 51 katika kituo cha umeme cha Kidatu, unarekebishwa ndani ya siku 15 ili kituo hicho kizalishe umeme kulingana na uwezo wake ambao ni megawati 204.

Dkt.Kalemani ametoa agizo hilo, tarehe 1 Machi, 2021 mara baada ya kukagua kituo hicho kilichopo mkoani Morogoro, na kukuta mtambo huo haufanyi kazi kutoka mwezi Septemba mwaka 2020.

 “ Nimetembelea eneo la mgodi na kukuta mashine moja kati ya nne zilizopo haizalishi umeme na nimefuatilia kwa watalaam wamesema bado wapo kwenye mchakato wa kununua spea ili wafunge kwenye mashine husika, kuna shida ya manunuzi hapa, kuna maafisa wamekalia kazi kutoka mwezi Septemba hadi sasa, jambo ambalo limeathiri upatikanaji umeme wa kutosha.”Amesema Dkt.Kalemani

Kutokana na hilo, Dkt.Kalemani amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, kuwachukulia hatua maofisa wawili wanaohusika na manunuzi, pamoja na  Meneja anayesimamia Kituo cha umeme cha Kidatu.

Aidha, akiwa kwenye kituo hicho, Dkt.Kalemani alikagua mitambo ya kupoza umeme na kukuta mashine moja haifanyi kazi kutoka Septemba 2020 na kuagiza kuwa, ndani ya mwezi mmoja ifungwe mashine mpya ili wananchi waweze kupata umeme wa uhakika na msimamizi wa mitambo hiyo achukuliwe hatua.

Vilevile, Dkt kalemani amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kuhakikisha kuwa matengenezo yoyote ya mitambo ya umeme nchini hayachukui zaidi ya siku Kumi.

Kuhusu vifaa vya kuzuia radi katika njia za usafirishaji umeme, Dkt. Kalemani ameiagiza TANESCO kununua vifaa hivyo ndani ya siku 17 ili hata mvua yenye radi inaponyesha, isiathiri upatikanaji wa umeme.

Akizungumzia hali ya maji katika Bwawa la Kidatu, Dkt.Kalemani amesema kuwa, bwawa hilo lina maji ya kutosha kuzalisha umeme unaotakiwa.

Katika ziara hiyo, Waziri wa Nishati aliambatana na  Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma, Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt.Tito Mwinuka na waatendaji wengine.