Chama cha Mapinduzi kimesimamisha uchapishaji wa gazeti la Uhuru kwa muda wa siku saba huku kikiwasimamisha kazi watendaji wakuu watatu wa gazeti hilo kwa madai ya upotoshaji wa kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Mapema leo chama hicho kilitoa taarifa kikieleza kusikitishwa na kitendo kilichofanywa na gazeti hilo cha kupotosha kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan iliyotokana na mahojiano ya kiongozi huyo na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), ambapo chama kiliahidi kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wote waliohusika katika uandaaji wa habari hiyo.
Gazeti hilo la CCM, toleo la leo Agosti 11, limeandika habari yenye kichwa kisemacho “Sina wazo kuwania urais 2025-Samia”, ambayo imepewa uzito mkubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari baadaye leo Jumatano Agosti 11, 2021, Katibu Mkuu wa chama hicho, Daniel Chingolo amesema uamuzi wa kuwasimamisha kazi viongozi hao umetolewa na bodi ambayo imeenda mbali na kuunda kamati ya kuchunguza sababu za jambo hilo kutokea.
“Ukifuatilia mahojiano aliyofanya Rais Samia Suluhu Hassan hakuna mahali alipozungumza maneno yaliyoandikwa kwenye kichwa cha habari cha gazeti la Uhuru la leo, amelishwa maneno na uungwana ni vitendo tunamuomba radhi Rais.
Viongozi waliosimamishwa kazi ni Mkurugenzi Mtendaji wa gazeti hilo, Ernest Sunguya ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Mhariri Mtendaji, Athumani Mbutuka na msimamizi wa gazeti hilo, Rashid Zahoro.
“Tumeamua mambo kadhaa, bodi ilikutana na kuleta taarifa ya hitimisho la kikao chao, ninaipongeza kwa uamuzi walioufanya na mimi kama Katibu Mkuu nimesimamisha kuanzia leo uchapishaji wa gazeti la Uhuru kwa siku saba, hayo ni mamlaka yangu,” amesema Chongolo.