Watu wanne wamefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa katika tukio la kurushiana risasi baada ya mtu mmoja ambaye hajafahamika kuwavamia polisi, kuwafyatulia risasi na kuwaua kisha kuchukua silaha katika maeneo ya daraja la Salenda karibu na Ubalozi wa Ufaransa, jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lililozua taharuki miongoni mwa wananchi limetokea leo Jumatano, Agosti 25, 2021 baada ya mtu huyo kufyatua hewani risasi huku akisikika akisema kuwa anawatafuta polisi. Akizungumza na wanahabari katika eneo la tukio, Mkuu wa Oparesheni Maalum za Kipolisi Liberatus Sabas amesema;
“Leo Agosti 25, 2021 tumekutwa na tukio la kiharifu, mtu mmoja ambaye hajafahamika alifika eneo ambapo walikuwepo askari wetu wakiwa kazini, akachomoa bastola na kuanza kuwashambulia kwa risasi na kusababisha vifo vya askari watatu ambapo askari polisi ni wawili na mmoja wa Kampuni ya SGA.
“Alichukua silaha na kuanza kurusha risasi hovyo, akaelekea karibu na Ubalozi wa Ufaransa huku akirusha risasi, amejeruhi watu sita. Askari wetu wamemdhibiti na kumuua. Hivyo jumla ya watu wanne wameuawa kutokana na tukio hilo.
“Kwa sasa ni mapema sana kujua nia yake ya kufanya hivyo lakini Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi,” amesema Kamanda Sabas.
Kamishna Sabas ameongeza kuwa watu sita wamejeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wanakoendelea kupatiwa matibabu, na kueleza kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi na utakapokamilika, taarifa itatolewa.