NEWS

23 Agosti 2021

Mahakama yatupilia mbali pingamizi la Utetezi Kesi Ya Ole Sabaya

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imetupilia mbali pingamizi la mawakili wa upande wa utetezi katika kesi ya unyang'anyi wakutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili.

Mawakili upande wa utetezi waliweka pingamizi dhidi ya Mawakili wa Jamhuri kumhoji mshitakiwa namba mbili, Sylvester Nyengu kuhusu nyaraka ambayo mshatikwa alisema Agosti 20 haitambui wakati wa utetezi.
 

Akitoa uamuzi huo mdogo  leo Agosti 23, 2021 hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo anayesikiliza kesi hiyo  amesema Mawakili wa upande wa Jamhuri wanaweza kuendelea kumhoji mshtakiwa.

"Katika sehemu ya hoja ya maswali ya dodoso  haina kikomo, shahidi au mshitakiwa anaweza kuulizwa maswali yoyote kuhusu kielelezo hatakama hakitambui," amesema Amworo.

Baada ya uamuzi huo Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka aliendelea kumhoji shahidi huyo kwa kutumia nyaraka hiyo.

Agosti 20, mwaka huu hakimu mwandamizi wa mahakama hiyo, Odira aliahirisha kusikiliza kesi hiyo baada ya mawakili wa utetezi kupinga uhalali wa wakili wa Jamhuri kumhoji shahidi huyo kupitia maelezo yanayodaiwa aliandika kituo cha polisi.

Awali kabla ya kuahirishwa kwa shauri hilo, kulitokea mvutano wa kisheria kwa mawakili wa pande zote mbili hali iliyomlazimu hakimu kuahirisha kesi kwa dakika 15 kwenda kupitia hoja za mawakili hao.

Hakimu mwandamizi wa mahakama hiyo, alidai mahakamani kwamba baada ya kupitia hoja hizo, na kufanya uchunguzi wake hakufikia mwisho kwa kuwa jambo hilo halikuwa dogo kama mawakili hao walivyodhani.

“Katika kupekuwa na kupitia hoja zenu nimeona kuna maswali mengi yamejitokeza, hivyo tunaahirisha kusikiliza shauri hili hadi Agosti 23, mwaka huu nitatoa uamuzi mdogo kwa kuwa pande zote zipo kwa ajili ya kutafuta haki,” alisema Hakimu Odira.

Akihojiwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, shahidi huyo wa utetezi alidai mahakamani huko, kwamba hakuwahi kuandika maelezo yoyote kituo cha polisi wala kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupata na Rushwa (TAKUKURU).

Katika hatua nyingine Wakili Kweka, aliiomba mahakama hiyo, kutumia kifungu namba 154 cha sheria ya ushahidi kutumia maelekezo ya shahidi aliyoandika kituo cha polisi kumhoji.

Wakili huyo wa Serikali, aliieleza mahakama kwamba kwa mujibu wa utaratibu wa kisheria maelezo hayo yanaweza kuwa  ya shahidi au kumhusu mwenyewe, pia siyo lazima maelezo  yawe yameandikwa na shahidi na wakati mwingine siyo lazima aonyeshwe maelezo hayo mahakamani kwa kuwa ni takwa la kisheria.