Shahidi namba nane upande wa Jamhuri katika kesi ya jinai Namba 105 ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili Mwalimu Magdalena (Zulfa) Mallya ameangua kilio mahakamani wakati akiielezea mahakama mazingira aliyokutana nayo wakati akimfuatilia mumewe shahidi namba sita Bakari Msangi aliyekuwa ametekwa na Sabaya na kundi lake.
Shahidi huyo ameieleza mahakama kuwa siku ya tukio Februari 9, 2021 akiwa nyumbani ambapo alidai alikuwa anaumwa yeye pamoja na mtoto wake, alikuwa akiwasiliana na mume wake kwa njia ya simu ila ilipofika kuanzia majira ya saa moja jioni mume wake hakuwa anapokea simu na baadaye hakuwa anapatikana kabisa jambo lililoanza kumpa wasiwasi kwani siyo kawaida ya mume wake kufanya hivyo.
Alidai ilipofika saa tano usiku simu yake iliita na alipoangalia alikuwa akipigiwa na mume wake ambaye alizungumza kwa sauti ya chini kama vile mtu aliyejificha mahali na kumwambia ameshikwa na Sabaya tangu saa 11 amepigwa na hali yake ni mbaya hivyo amfuate.
"Nikiwa pale hoteli ya Tulia jirani alienda kuulizia mume wangu akaambiwa hayupo tukageuza gari tukawa tunataka kutoka nje ili tuone tunapataje msaada hata wa polisi wakati anageuza ghafla simu yangu iliita mume wangu aliongea kwa maumivu makali sana akasema usiindoke nikamwambia si ushuke akaniambia amefungwa pingu miguuni....kwa kweli niliumia sana,"alisimulia shahidi huyo huku akilia .
Shahidi huyo aliendelea kueleza mahakama hiyo kuwa walibaki ndani ya eneo hilo ambapo baada ya muda alimuona Sabaya akitoka ndani ya hoteli hiyo akiwa ameshika bastola na bahasha ya kaki na alipoingia kwenye gari na vijana wake kwenye magari mengine magari yaliwashwa kwa ajili ya kuondoka.
"Nikakimbilia getini nikapiga magoti na nilikuwa nimenyoosha mikono nikaita mheshimiwa naomba usimuue mume wangu tuna watoto wadogo na mimi ni mgonjwa, ninakuomba mheshimiwa muachie mume wangu na Mungu atakubariki nilipiga kelele sana gari yake ikashika breki pale nilipopiga magoti,"aliendelea huku akilia.
6 Agosti 2021
Home
Unlabelled
Shahidi kesi ya Ole Sabaya aangua kilio mahakamani.