Na Mbaraka Kambona,
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel amekutana na Ujumbe kutoka nchini Saudi Arabia kwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara ya nyama na nchi hiyo.
Prof. Ole Gabriel alikutana na Ujumbe huo kutoka Saudi Arabia ulioongozwa na Mkaguzi, Mamlaka ya Dawa na Chakula, Saudi Arabia, Ahmed Alhajouj jijini Dar es Salaam jana.
Kwa mujibu wa Prof. Gabriel kabla ya kukutana nao, ujumbe huo ulipata fursa ya kukagua maeneo mbalimbali yanayohusika na uchakataji wa mazao ya mifugo ikiwemo Machinjio, Maabara na Shirika la Viwango Tanzania(TBS) ambapo kote wamejirisha na kutoa mapendekezo kadhaa ya kuboresha ili biashara hiyo iweze kufanyika kwa viwango vinavyohitajika na nchi hiyo.
Alisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameielekeza Wizara hiyo kutafuta masoko nje ya nchi hivyo Wizara inaendelea kufanya jitihada ikiwemo hatua hiyo ya kutafuta soko katika nchi Saudi Arabia.
"Haya masoko ya nje ya nchi ni mazuri kwa sababu yanatupatia fedha za kigeni lakini pia yanawahakikishia wafugaji wetu soko la uhakika kwa mazao ya mifugo yao," alisema Prof. Ole Gabriel
Aidha, Prof. Gabriel alitoa rai kwa Wafugaji nchini kuchukulia hatua hiyo kama ni fursa kubwa na hivyo wahakikishe wanaboresha ufugaji wao kuwa wa kisasa zaidi ili kukidhi soko hilo la kimataifa.
"Serikali ni rahisi kutafuta masoko lakini je, mifugo iliyopo inakidhi soko hilo? hivyo niwaombe wafugaji na Wafanyabiashara watumie fursa hii vizuri ili kuboresha uchumi wao na wa Taifa pia," aliongeza Prof. Ole Gabriel
Alisema Sekta ya Mifugo kwa sasa inachangia katika pato la Taifa kwa asilimia 7.4 lakini lengo la Wizara ni kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2025 na hilo linawezekana kama milango ya masoko nje ya nchi ikianza kufunguka kwa uhakika.
Prof. Ole Gabriel aliongeza kuwa wao kama wizara watatoa ushirikiano kwa kila mdau anayechangia katika mnyororo wa thamani wa mazao ya mifugo kuhakikisha kunakuwa na mazao bora kwa ajili ya soko la ndani na la nje.
Naye, Msajili wa Bodi ya Nyama, Dkt. Daniel Mushi alisema anaishukuru Serikali kwa jitihada mbalimbali inazozifanya kwa kushirikiana na wadau kufungua masoko mengine nje ya nchi ili kuuza nyama katika masoko yanayolipa bei nzuri.
Aliongeza kuwa ujio wa ujumbe huo umewapa changamoto kwani kuna mambo wanapaswa kufanya ili nyama ya Tanzania iweze kukubalika katika masoko ya nje.
Aliendelea kusema kuwa ili waweze kufikia masoko hayo ni lazima kuboresha lishe ya mifugo ili wanyama waweze kukua kwa haraka na ambao watakuwa na nyama nyingi yenye ubora.
Itakumbukwa hivi karibuni, Rais Samia alikutana na Mtoto wa Mfalme wa Saudi Arabia ambapo miongoni mwa maeneo yaliyoangaliwa ni pamoja na Sekta ya Mifugo na aliielekeza Wizara kutafuta masoko nje ya nchi ikiwemo nchi ya Saudi Arabia.