NEWS

10 Agosti 2021

Tanzania Yasaini Mkataba Wa Uanzishwaji Wa Taasisi Ya Udhibiti Wa Dawa Ya Umoja Wa Afrika


 Tanzania imesaini Mkataba wa uanzishwaji wa Taasisi ya Udhibiti wa Dawa ya Umoja wa Afrika (African Medicines Agency) na kuwa Nchi ya 22 kusaini Mkataba huo unaohusisha Nchi Wanachama.
 
Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini Mkataba huo katika Ofisi za Makao Makuu za Umoja wa Nchi huru za Afrika (AU) zilizopo Addis Ababa nchini Ethiopia, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, amesema lengo la Tanzania kusaini mkataba huo ni kuunganisha nguvu na jitihada za pamoja na nchi nyingine za Afrilka katika kupambana na dawa bandia na duni.
 
Ameongeza kuwa Taasisi hiyo ya Udhibiti wa Dawa ya Umoja wa Afrika (African Medicines Agency) kwa kifupi AMA itasaidia katika kuunganisha jitihada za taratibu za kuwianisha (harmonization) mifumo ya udhibiti wa dawa katika Jumuiya za kiuchumi za kikanda Barani Afrika akitolea mfano chanjo mbalimbali ikiwemo ya UVIKO 19.
 
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Bwana Adam Fimbo, amesema uwepo wa Taasisi ya AMA utawezesha kupatikana kwa soko la dawa nchini Tanzania kuendana na Mkataba wa Afrika wa maeneo huru ya kibiasahara pamoja na kuwezesha upatikanaji wa haraka wa dawa wakati wa dharura pamoja na majanga ambapo kwa sasa Tanzania ina takribani viwanda vipya 17 vya dawa vilivyopo katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji.
 
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Dkt. Monica Nsanzabaganwa, amesema kuwa Taasisi ya AMA ni muhimu hasa katika kuweka mifumo imara ili kuwezesha nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kutatua kwa pamoja changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta ya afya.
 
Taasisi ya Udhibiti wa Dawa ya Umoja wa Afrika (AMA) inatarajiwa kuanza rasmi kufanya kazi mwaka 2022 baada ya kusainiwa na jumla ya nchi 27 za Umoja wa Afrika ambapo mpaka sasa nchi 22 zimesaini ikiwemo Tanzania ambayo ilipaswa kusaini mkataba huo tangu Februari 2020 lakini kutokana na janga la UVIKO 19 zoezi hilo liliahirishwa.