NEWS

23 Agosti 2021

Waziri Mkenda Alivyoongoza Mamia Ya Wananchi Mazishi Ya Basil Mramba


Na Mathias Canal, Rombo-Kilimanjaro
Mamia ya wananchi wa Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro na kwingineko nchini wamejitokeza kuuaga mwili wa aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Rombo na kushika wadhifa mkubwa akihudumu wakati huo kama waziri wa fedha, Mhe Basil Pesambili Mramba.

Katika shughuli hiyo ya kuaga mwili huo iliyofanyika katika viwanja vya sabasaba vilivyopo katika Halamshauri ya wilaya ya Rombo kwa niaba ya serikali, iliongozwa na Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda aliyemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan.

Mhe Mramba ambaye alifariki Agosti 17, mwaka huu katika hospitali ya Regency iliyopo mkoani Dar es salam ameagwa katika uwanja wa sabasaba na kisha kuzikwa kijijini kwake Shimbi wilayani Rombo.

Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Rais Samia,  Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda ambaye amesema Taifa litamkumba Basil Mramba kwa uzalendo na juhudi zake alizozifanya wakati akiwa katika nyadhifa mbalimbali za uwaziri serikali na kusema ameacha alama kubwa kwa Taifa inayopaswa kutambuliwa ipasavyo.

Waziri Mkenda amesema kuwa, Mramba ameacha alama ambazo hazitafutika kamwe katika wilaya ya Rombo hasa katika suala la barabara na kilimo cha ndizi na maparachichi ambacho ndio uchumi mkubwa na tegemezi kwa wananchi wa wilaya hiyo.

"Wananchi wa Rombo kamwe hatutamsahau Mramba kwa mambo makubwa aliyoyafanya wakati wa ubunge wake,wakati anaingia kwenye ubunge kwa mara ya kwanza Rombo ilikuwa na shule nne pekee za Sekondari na mpaka anaondoka kwenye nafasi hii ya ubunge alicha shule zaidi ya 40 kutokana upambanaji wake," Amekaririwa Profesa Mkenda

Waziri huyo wa Kilimo Mhe Profesa Mkenda amewaahidi wananchi wa Jimbo hilo kuwa ataendeleza yale yote ambayo Mramba alitamani kuyakamilisha lakini hayakukamilika wakati alipouwa madarakani.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kilimanjaro, Ndg Patrick Boisafi amesema kifo cha Mramba ni pigo kubwa kwa wanachi na wakazi wa Rombo na Taifa kwa ujumla kwani alikuwa ni mtu aliyetumikia Taifa kwa upendo na kulipenda jimbo lake.

"Mramba ameacha alama hapa Rombo na Taifa kwa ujumla, maisha yake yanajieleza na alifanya kazi kubwa kwenye nchi hii na sisi sote ni mashahidi, aliipenda Rombo na Kilimanjaro kwa ujumla tuna cha kujifunza  kupitia kwake, alitumia nafasi aliyopewa na serikali kuwatumikia wananchi wake," Amesema Boisafi

Akizungumza wakati wa ibada ya mazishi, Mwakilishi wa Askofu wa jimbo katoliki la moshi, Padre Deogratius Matiika amesema Mramba ameandika historia katika jimbo hilo na kwa kanisa katoliki na kwamba atakumbukwa kwa mengi kwani alikuwa ni kimbilio la wengi.

"Tutaendelea kumuenzi ndugu yetu Mramba amekuwa ni mti mzuri uliozaa matunda kwani alimpenda Mungu na alimtumikia ipasavyo, alishiriki nasi katika maeneo mbalimbali pale ambapo kulikuwa na msaada kanisani alitusaidia, ameandika historia ambayo haitafutika Kilimanjaro, hakuna anayeweza kupinga hili kwamba aliweka historia wilaya ya Rombo," Amesisitiza Padre Matiika

Mramba alihudumu katika nyadhifa mbalimbali za uwaziri ikiwemo Waziri wa Fedha, Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye pia alikuwa mwanzilishi wa viwanda vidogo vidogo nchini (SIDO)