Na Angela Msimbira, NJOMBE
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Ummy Mwalimu ameanza ziara ya kikazi leo mkoani Njombe ambapo pamoja na mambo mengine atakagua miradi ya maendeleo kwenye sekta ya afya ngazi ya msingi, sekta ya elimu na ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Akizungumza Agosti 10,2021 na Sekretarieti ya Mkoa huo, Waziri Ummy ameupongeza uongozi na watendaji kwa kuendelea kwa kasi, ari na jitihada katika kutatua changamoto mbalimbali za kimaendeleo na kuongoza kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mwaka 2021/2022.
Amesema Sekretarieti za Mikoa zina wajibu wa kuhakikisha Halmashauri zote nchini zinatimiza majukumu yao kikamilifu kwa kuwa wananchi wanahitaji kupatiwa maendeleo na maendeleo yanapatikana kwa Halmashauri imara.
Katika ziara hiyo, Waziri Ummy amesisitiza umuhimu wa viongozi wa sekretarieti za Mikoa nchini kuhakikisha wanasimamia kwa weledi ukusanyaji na matumizi ya mapato ya ndani kwa kuwa ndio wasimamizi wakuu katika ngazi ya Halmashauri.
Aidha, amesema kuwa Makatibu Tawala wasaidizi wa Mikoa wana wajibu wa kuhakikisha wanachambua bajeti za halmashauri na kuangalia vipaumbele ambavyo vinasaidia katika kutatua kero za wananchi zikiwemo ununuzi wa madawati, ujenzi wa vyumba vya madarasa, ujenzi wa vituo vya afya na Hospitali za Wilaya na ujenzi wa miundombinu ya Barabara.
“Makatibu Tawala wasaidizi wa Mkoa wanawajibu wa kuhoji na kuchambua bajeti za Halmashauri kwa kina, kwa kuangala vipaumbele vitakavyosaidia kutatua kero za hasa katika masuala ya elimu, afya na miundombinu kwa ujumla. Ni kazi yenu kufanya kazi hiyo na sio ofisi ya Rais TAMISEMI, Ni wajibu wenu kusimamia matumizi ya Halmashauri kwa kuhakikisha fedha zinapelekwa katika kutatua kero za wananchi,”amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Ummy amewaagiza Wakurugenzi wote nchini kuhakikisha wanatenga fedha za makusanyo ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotatua kero za wananchi.
Kabla ya kikao na Sekretarieti ya Mkoa, Waziri Ummy amekutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya na kukutana na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi(CCM).