Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro, amewataka wanasiasa kuendelea kufuata sheria za nchi na kufanya siasa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo na kuendelea kujiepusha kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani kwani kufanya hivyo sheria itaendelea kuchukua mkondo wake ikiwemo kufikishwa mahakamani.
IGP Sirro amesema hayo wakati akifungua zahanati ya Polisi mkoni Katavi ambayo hadi kukamilika kwake imegharimu jumla ya kiasi cha shilingi milioni 103 ambapo pia amewataka watendaji watakaokuwa wakitoa huduma kwenye zahanati hiyo kutoa huduma bora kwa wateja na kwa kuzingatia usiri kati ya mtoa huduma na mgonjwa.
Aidha, IGP Sirro amesema kuwa, hadi sasa hali ya ulinzi na usalama nchini imeendelea kuimarika licha ya kuwepo kwa matukio machache hasa ya uporaji wa kwenye barabara kuu ambayo mpaka sasa yamedhibitiwa na wahalifu wamekamatwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Katavi, Mkuu wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph amesema kuwa, zahanati ya Polisi ni miongoni mwa zahanati zilizopo kwenye wilaya hiyo ambayo inatoa huduma zinazoendana na wakati kutokana na ubora wa huduma, vifaa na wataalam na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kupata huduma kwenye zahanati hiyo.