Na Mary Gwera, Mahakama-Tanga
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewahimiza Wadau wa mnyororo wa utoaji haki nchini kusoma hukumu zinazotolewa na Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ambazo zimesheheni mambo muhimu yatakayosaidia kurahisisha utoaji wa haki kwa wananchi ikiwa ni pamoja na namna bora ya kushughulikia mashauri ya Mirathi na ya dawa za kulevya.
Akizungumza kwa nyakati tofauti siku ya kwanza ya ziara yake ya kukagua shughuli za Mahakama Kanda ya Tanga aliyoianza jana tarehe 16 Mei, 2022 akiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Wilaya ya Pangani, Mhe. Prof. Juma alisema kuwa kwa kufanya hivyo itapunguza baadhi ya makosa yanayofanywa na wadau wakiwemo waendesha mashtaka na wananchi kwa kutojua sheria na kanuni zinazosimamia mashauri mbalimbali.
“Mahakama ya Tanzania kwa sasa inafanya kazi zake kwa uwazi, uamuzi wa mashauri mbalimbali ya Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu huwa tunapandisha katika mtandao wetu wa TanzLII unaopatikana katika tovuti yetu ya www.judiciary.go.tz, hivyo ni rai yangu kwa wananchi kuzisoma na hatimaye kutorudia makosa yanayojitokeza mara kwa mara,” amesema Jaji Mkuu.
Aidha, Mkuu huyo wa Mhimili wa Mahakama, alibainisha miongoni mwa mashauri yaliyopo kwa wingi mkoani Tanga ni pamoja na Mashauri ya Dawa za kulevya, Mirathi na ya unyanyasaji wa kijinsia.
“Kabla ya kuanza ziara hii, mimi pamoja na Majaji wenzangu tulikuwa hapa (Tanga) katika vikao maalum vya Mahakama ya Rufani, nilichogundua ni kwamba asilimia kubwa ya mashauri yaliyopo kwa wingi ndani ya Mkoa huu ni ya Dawa za kulevya, Mirathi na unyanyasaji wa kijinsia,” alisisitiza Mhe. Prof, Juma.
Aliongeza kwa kuwakumbusha Majaji, Mahakimu na Waendesha Mashtaka wanaosimamia mashauri mbalimbali kuzingatia sheria na taratibu ili haki itendeke.
“Mathalani katika mashauri ya Mirathi kwa muda sasa kumekuwa na changamoto ya mashauri hayo kuchukua muda mrefu na vilevile Wasimamizi wa Mirathi kujigeuza kuwa Wamiliki wa mali, hali hii inatakiwa idhibitiwe na mashauri yanatakiwa kukamilika ndani ya miezi sita (6),” alisema Jaji Mkuu.
Katika hatua nyingine, akizungumza kuhusu matumizi ya TEHAMA, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma alisema kuwa safari ya matumizi hayo kuelekeza Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’ bado inaendelea hivyo ameagiza kuwa Viongozi wa Kanda, mikoa na Wilaya za Mahakama ni vyema waendelee kusimamia thabiti ili kwenda sambamba na dunia inakoelekea.
“Hivi sasa kama mnavyofahamu kuna zoezi la kuweka anuani za makazi, kuweka postikodi hayo yote ni matayarisho ya uchumi ambao unahama, unakuwa uchumi wa kidijitali, sasa ule uwekezaji utatusaidia kwenda kwenya Mahakama mtandao na tunapoenda Mahakama mtandao sio Mahakimu na Majaji pekee ndio waende kule ni watumishi wote waende kwenye Mahakama mtandao hivyo ni muhimu wote tujitayarishe kuhama kwa kuwajengea uwezo watumishi wote,” alisisitiza.
Aliongeza kwa kutoa agizo kwa Watendaji wa Mahakama nchini kuhakikisha wanahuisha taarifa za Mahakama ndani ya wiki mbili kuanzia sasa kwa Mahakama kuwa na anuani za makazi pamoja na kuhuisha taarifa za msingi hata katika barua zetu za kuitwa mahakamani ‘summons’ ili ziwe rahisi kufika kwa mhusika kwa wakati muafaka.
Katika ziara hiyo, Jaji Mkuu anatarajia pia kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Wilaya za Kilindi, Handeni, Lushoto na Korogwe kabla ya kuhitimisha ziara yake Tanga mjini.