Halmashauri kuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi, imemsimamisha Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, James Mbatia na Makamu Mwenyekiti wake Bara, Angelina Mtaigwa, kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo ukiukwaji wa maadili.
Uamuzi huo umetangazwa Jumamosi, tarehe 21 Mei 2022 na Mwenyekiti wa kikao cha halmashauri hiyo kilichoketi jijini Dar es Salaam, Joseph Selasini.
Akisoma maazimio ya halmashauri hiyo, Selasini amedai Mbatia amesimamishwa katika wadhifa huo kutokana na kutokuwa na mahusiano mazuri na makatibu wake.
Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Martha Chiomba, alidai kulazimishwa kujiuzulu na Mbatia, tuhuma ambazo mwanasiasa huyo alizikanusha.
“Tulielezwa jinsi ambavyo mwenyekiti alimtaka katibu mkuu ajiuzulu na ikumbukwe hana zaidi ya mwaka ndani ya chama na katika mjadala tumekubaliana alikuwa anabadilisha makatibu wakuu jinsi anavyotaka. Sasa huyu ni katibu wa sita tangu alivyokuwa mwenyekiti,” amedai Selasini.
Selasini ametaja sababu nyingine za Mbatia kusimamishwa, akidai anatuhumiwa kwa kukisabisha chama hicho kisishiriki mikutano mbalimbali iliyotitishwa kwa ajili ya kujadili masuala ya demokrasia ya vyama vingi, ikiwemo ulioitishwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Amedai, awali chama hicho kilikataa kushiriki vikao hivyo hadi Serikali itakapokuwa na nia njema dhidi ya viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani, ikiwemo kuachwa huru kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyekuwa rumande katika Gereza la Ukonga, kwa tuhuma za ugaidi.
Selasini amedai, baada ya Mbowe kuachwa huru Machi 2022, NCCR-Mageuzi haikuwa na kikwazo cha kushiriki vikao hivyo lakini Mbatia aliitisha kikao cha kamati cha dharura kubatilisha uamuzi huo.
Selasini amedai maazimio ya halmashauri hiyo kumsimamisha Mbatia ni halali, kwani akidi ya wajumbe wake ilikidhi matakwa ya kisheria ambapo waliohudhuria ni 52 kati ya wajumbe 82.
“Kabla ya mjadala haujaanza ulizuka mjadala wa Mwenyekiti wa chama kutokuwepo katika mkutano huu na taarifa ilitolewa kwamba anazo taarifa za mkutano akishiriki kuuitisha na baada ya kusubiri kwa muda bila kujulikana na wajumbe wako tayari ukumbi tukaona mkutano uendelee,” amesema Selasini.