Rais Vladimir Putin wa Russia ametetea oparesheni za kijeshi ambazo nchi yake ilianzisha dhidi ya Ukraine na kusema ilibidi afanye hivyo kwani nchi za Ulaya zilikuwa zinapanga kuishambulia Russia kijeshi.
Putin ameyasema hayo katika hotuba wakati wa gwaride la kila mwaka la Siku ya Ushindi katika Medani Nyekundu mjini Moscow leo Jumatatu kwa munasaba wa kukumbuka ushindi wa Shirikisho la Sovieti dhidi ya Ujerumani ya Kinazi katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Akifafanua zaidi, Rais Putin amesema: "Nchi za Magharibi zilikuwa zinajitayarisha kuvamia ardhi yetu, likiwemo eneo la Crimea, na hivyo oparesheni ya kijeshi (nchini Ukraine) ilikuwa hatua ya kuzuia uvamizi."
Putin amesema nchi za muungano wa kijeshi wa NATO zilikataa kusikiliza ilichokuwa ikikisema Russia jambo lililoashiria zilikuwa zinapanga njama na kwa msingi huo Russia ilichukua uamuzi wa kuzuia hujuma dhidi yake huku akisema uamuzi wake wa oparesheni za kijeshi nchini Ukraine ulikuwa wa nguvu na kwa wakati muafaka.
Aidha amesema uamuzi huo wa oparesheni za kijeshi dhidi ya Ukraine ulikuwa sahihi kwani nchi hiyo ilikuwa inapokea silaha za kisasa kabisa kutoka muungano wa kijeshi wa NATO.
Rais wa Russia amefichua kuwa Ukraine ilikuwa inapanga kujizatiti kwa silaha za nyuklia na hivyo nchi yake haikuwa na budi ila kuanzisha oparesheni za kijeshi dhidi ya Kiev ili kusambaratisha njama hizo.
Russia ilianzisha oparesheni za kijeshi dhidi ya Ukraine mwezi Februari baada ya nchi hiyo kukataa kutekeleza mapatano ya Minsk na pia baada ya maeneo ya Donetsk na Luhansk kujitangazia uhuru ambao ulitambuliwa rasmi na Moscow.