NEWS

10 Mei 2022

Rais Samia Asikia Kilio cha Bei ya Mafuta....Atoa Maelekezo Mazito


Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza mkakati wa kubana matumizi ya Serikali katika bajeti ya matumizi ili kupata fedha za kupunguza makali ya ongezeko la bei ya mafuta linalosababisha kuongezeka kwa bei za bidhaa na huduma nchini.

Rais Samia ameyasema hayo jana Jumatatu Mei 9, 2022 katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari akisema Serikali imesikia kilio cha wananchi cha kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo.

“Katika mwaka wa fedha unaoanza Julai mwaka huu tutachukua hatua mbalimbali za kikodi kuweka ahueni kwa wananchi.

“Hata hivyo, kutoa nafuu za kupanda kwa bei za mafuta hakuwezi kusubiri hadi mwaka huu wa fedha, nimeamua kwa hiyo wananchi waanze kupata nafuu kuanzia tarehe Mosi Juni.

Nimeelekeza kwamba, Serikali tujibane na tujinyime ili kupata fedha kutoka kwenye matumizi ya kawaida ya Serikali ili ziende kutoa nafuu za bei ya mafuta kuelekea mwaka wa fedha,” amesema Rais Samia.

Amemwagiza Waziri wa Nishati kutoa ufafanuzi kesho Bungeni kuhusu hatua hiyo, huku akimwelekeza Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kutoa ufafanuzi wa kodi katika mafuta.

Amesema ongezeko la bei ya mafuta limetikisa nchi zote duniani, tajiri na masikini, zenye kuzalisha mafuta na zenye kuagiza na kwamba Tanzania haijasalimika.

“Novemba mwaka jana nilielekeza tupunguze tozo zinazotozwa na taasisi mbalimbali. Hatua hiyo ilisababisha Serikali kupungukiwa kwa mapato yake kwa kiasi ccha Sh102 bilioni.

Pamoja na hatua hizo bado nafuu haikupatikana kutokana na kasi ya kupanda bei,” amesema.