NEWS

9 Mei 2022

Russia: Tuna uwezo wa kuziharibu nchi za NATO katika kipindi cha nusu saa tu!


Mkuu wa Taasisi za Anga za Mbali ya Russia ametoa onyo kali kwa nchi wanachama wa NATO na kusema kuwa, kama kutazuka vita vya nyuklia, basi Moscow inaziharibu nchi za NATO katika kipindi cha nusu saa tu.

Mkuu wa Taasisi za Anga za Mbali ya Russia ametoa onyo kali hilo kwa nchi wanachama wa Muungano wa Kijeshi wa nchi za Magharibi (NATO) baada ya nchi hizo kuendelea na chokochoko zao dhidi ya Moscow. 

Onyo hilo lilitolewa jana baada ya Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg kutishia juzi Jumamosi kuwa wanaweza kutumia silaha za atomoki kukabiliana na Russia.

Onyo hilo kali la Moscow la kuziangamiza nchi wanachama wa NATO katika kipindi cha nusu saa tu limetolewa baada ya Wizara ya Ulinzi ya Russia kusema kuwa imefanikiwa kuharibu idadi kubwa ya silaha na zana za kivita ambazo Ukraine imepokea kutoka Marekani na Ulaya.

Taarifa ya Jumamosi ya wizara hiyo imesema silaha hizo zilikuwa katika maeneo ya Kharkiv na bandari ya Odesa nchini Ukraine. Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zimekuwa zikiipa serikali ya Ukraine idadi kubwa ya silaha zinazotumika kukabilia na jeshi la Russia.

Huku vita vya Ukraine vikiwa vinaingia siku yake ya 74 mkuu wa kamandi ya Majeshi ya Ufaransa Jenerali Thierry Burkhard amesema nchi za Magharibi zinapaswa kujitayarisha kwa uhasama wa muda mrefu na Russia. 

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov amesema, vikwazo vya Magharibi havina athari yoyote kwa  nchi hiyo.

Baada ya Russia kuanzisha operesheni ya kijeshi ndani ya ardhi ya Ukraine tarehe 24 Februari 2022, Marekani na nchi nyingine za Magharibi zilianza kuiwekea Moscow vikwazo vikubwa vya pande zote.

Credit:Parstoday