Na. Saidina Msangi, WFM, Arusha
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha kuwa taasisi zote za umma zinatumia Mfumo wa Ununuzi kwa Njia ya Mtandao (TANePS) na hatua kali zichukuliwe dhidi ya maafisa masuuli ambao taasisi zao zitakaidi matumizi ya mifumo katika ununuzi wa umma.
Maagizo hayo aliyatoa jijini Arusha, wakati akifungua kongamano la Wiki ya ununuzi wa Umma lililowakutanisha wadau wa ununuzi takribani 1000 wakiwemo maafisa ugavi, wazabuni, wajumbe wa bodi na maafisa masuuli kutoka Wizara, taasisi, Halmashauri na sekta binafsi.
Akizungumza katika kongamano hilo Mhe. Majaliwa alisisitiza matumizi ya mifumo katika ununuzi wa umma pamoja na kuhakikisha ufanisi wa mifumo hiyo ili huduma zipatikane kwa wakati ukiwemo umakini wa wanaosimamia mifumo na kuwa na njia mbadala ikitokea changamoto ya mtandao.
‘Wizara ya Fedha na Mipango ifanye tathmini na maboresho ya mifumo na taratibu za ununuzi ili kudhibiti mianya iliyopo inayosababisha Serikali kupoteza fedha nyingi kwa huduma ambazo kiuhalisia bei zake ni za chini,’ alisema Mhe. Majaliwa.
Alisisitiza kuwa ili kupata thamani halisi ya fedha katika ununuzi wa umma usimamizi madhubuti unahitajika katika sekta hiyo hasa kwa kuzingatia kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Bajeti ya Serikali ambayo inatokana na fedha za walipa kodi, inatumika katika ununuzi wa bidhaa, huduma na kandarasi za ujenzi.
Alisema kuwa kipindi kinachoishia Machi 2022 jumla ya zabuni 48,487 zenye thamani ya Sh. trilioni 22.7 zimechakatwa, hivyo fedha hizo zinazotumika kwenye ununuzi zinahitaji usimamizi madhubuti kwa kuwa kinahusisha matumizi ya fedha za walipa kodi.
Pia Mhe. Majaliwa aliiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kupitia kitengo chake cha Usimamizi wa Mifumo ya Taarifa za Kifedha na GPSA ihakikishe bei zote za bidhaa na huduma zinazotumika sokoni kwa jumla na rejareja zinaingizwa kwenye mfumo wa TANEPS na kuwa na kiwango cha ukomo wa bei zitakazotumika Serikalini.
Aidha amewataka wadau wa kongamano la Wiki ya ununuzi wa umma kutumia wiki hiyo kuendelea kuhamasishana, kupeana uzoefu na pia kujadiliana namna bora zaidi ya kuendelea kutumia teknolojia kuboresha ununuzi wa umma nchini, pamoja na kuelimisha wananchi umuhimu wa teknolojia katika manunuzi ya umma.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), katika kongamano hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) alisema Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha sekta ya ununuzi wa umma kwa maslahi ya Taifa kwa kufanya maboresho katika Sheria ya ununuzi wa umma.
Alisema maboresho hayo ni pamoja na kurekebisha vifungu vilivyokuwa vinakwamisha utekelezaji wa ununuzi kwa ufanisi na kuhakikisha kuwa sekta ya ununuzi inawashirikisha watanzania wa makundi yote katika kujenga uchumi wa Taifa.
‘Faida zilizotokana na marekebisho ya Sheria ni pamoja na kupungua kwa muda wa mchakato wa ununuzi, ushughulikiaji wa malalamiko ya wazabuni, upendeleo kwa makampuni yanayomilikiwa na watanzania na upendeleo kwa makundi maalumu ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu’ alisema Mhe. Chande.
Alisema kuwa Serikali imeendelea na jitihada za kuimarisha utekelezaji wa ununuzi wa umma nchini kwa kuanzisha na kusimamia utekelezaji wa mifumo ya kielektroniki katika kudhibiti matumizi na kuongeza ufanisi kwenye ununuzi wa umma.
Aidha, Mhe. Chande alieleza kuwa wiki ya ununuzi wa umma inatoa fursa kwa wadau wa ununuzi wa umma na ugavi kubadilishana uzoefu pamoja kufanya maonesho ya huduma wanazotoa kwa jamii.
Kongamano la Wiki ya ununuzi wa Umma limeandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango na taasisi zinazosimamia ununuzi wa umma nchini ambazo ni Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA), Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA) na Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB).