NEWS

16 Mei 2022

Urusi: Tumeteketeza vituo 104 vya kiijeshi vya Ukraine hadi hivi sasa


Wizara ya Ulinzi wa Russia imetangaza kuwa, hadi hivi sasa operesheni maalumu ya kijeshi ya nchi hiyo huko Ukraine iimeshateketeza vituo 104 vya kijeshi vya Ukraine.

Shirika la habari la TASS la Russia limemnukuu Igor Konashenkov, Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo akisema hayo leo (Jumatatu) na kuongeza kuwa, mbali na kuteketeza vituo hivyo 104 vya kijeshi vya Ukraine, jeshi la Russia limeteketeza pia vituo vitatu vikuu vya komandi za kijeshi na maghala mawili ya mafuta ya kuendeshea zana za kijeshi za Ukraine.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jeshi la ulinzi wa anga la Russia limetungua pia ndege mbili za Ukraine aina ya Sukhoi-25 katika sehemu ya Kalininskoye ya eneo la Nikolayev kama ambavyo jeshi hilo limeharibu pia ndege 10 zisizo na rubani za Ukraine katika jimbo la Donetsk.

Taarifa zinasema kuwa, tangu ilipoanza operesheni maalumu ya kijeshi ya Moscow tarehe 24 mwezi Februari mwaka huu huko Ukraine, majeshi ya Russia yameshateketeza ndege 168 za kijeshi za Ukraine, ndege 889 zisizo na rubani pamoja na vifaru na magari ya deraya 3,108 ya Ukraine.

Russia inasema kuwa imeamua kuanzisha operesheni maalumu ya kijeshi huko Ukraine si kwa lengo la kuikalia kwa mabavu nchi hiyo, bali ni kwa ajili ya kuipokonya silaha, kudhoofisha nguvu zake za kijeshi na pia kuzuia vita vikubwa kati yake na madola ya Magharibi hasa kutokana na chokochoko za nchi za Magharibi ambazo zimedharau wasiwasi mkubwa wa Russia wa kuzitaka nchi hizo zisijizatiti kijeshi kwenye mipaka yake.