NEWS

23 Machi 2017

Harmorapa Atimua Mbio Baada ya Kuiona Bastola Aaliyotishiwa Nape..!!!


Harmorapa ni bingwa wa kumendea headlines kwenye matukio makubwa yanayowahusu watu wenye majina. Hata hivyo Alhamis hii mambo yalitaka kumtokea puani.

Rapper huyo mwenye visa alitimba Protea Hotel jijini Dar es Salaam ambako mheshimiwa Nape Nnaye alikuwa ameenda kuzungumza na waandishi wa habari, lengo lake kumpa pole kwa masahibu yaliyompata – kuvuliwa uwaziri.

Hata hivyo wakati anakimbia kwenda kumpa mkono wa pole Nape aliyekuwa kwenye kukuru kukara na wana usalama wasiokuwa na magwanda waliokuwa wakimzuia waziri huyo wa zamani kutimiza azma yake, macho ya Harmorapa yalitua katika chombo cha hatari chenye uwezo wa kutoa pumzi ya mwanadamu – bastola aka cha moto na kujikuta akitimua mbio kuokoa maisha yake.

Video inaonesha mwanausalama huyo akichomoa cha moto na kuwafanya watu waliokuwa jirani kupata hofu ingawa ni Harmorapa ndiye aliyeonesha kuogopa zaidi kiasi cha kutamani kupaa kutoka kwenye eneo hilo.

Haijulikani ‘Kiboko huyo wa Mabishoo’ alisimamia wapi baada ya kutimua mbio hizo, lakini mashuhuda waliokuwepo wanatonya kuwa jamaa alilala mbele kwa speed za Usain Bolt – chezea bastola wewe!

Kutokana na kitisho hicho, Harmorapa alishindwa kumpa mkono wa pole mheshimiwa Nape japo alifanikiwa kupata interview mbili tatu za waandishi waliomshuhudia – mission accomplished.

Hiyo si mara ya kwanza kwa mkali huyo wa social media kutinga kwenye matukio ya watu wengine na kuchukua spotlight. Hivi karibuni rapper huyo alienda pia kwenye studio za Clouds FM kuwapa pole baada ya studio zao kuvamiwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam.