Ndugu zangu,
Habari kubwa leo ni Nape Nnauye. Ameondoka kwenye Baraza la Mawaziri.
Kwa tunaofuatilia mambo hii ni habari iliyokuja kwa kuchelewa. Kwangu mimi ni siku ile Rais wa Jamhuri alipoongea Ubungo kwamba Mkuu wa Mkoa Makonda aendelee kuchapa kazi, na baadae Waziri wake wa Habari anatangaza tume kumchunguza Makonda. Nape angemsaidia Rais kwa kuvunja alichokiunda kwa maana ya Tume. Kisha kujiuzuru, basi.
Maana, kwenye Jamhuri, hakuna uwezekano wa jambo kama lile kufanywa na Waziri na akabaki kuwa Waziri. Nape ambaye alipaswa, Kama Waziri wa Habari, kuwapo pia kwenye tukio kubwa kitaifa kama lile la uzinduzi wa ujenzi wa flyovers pale Ubungo mbele ya Rais wa Benki ya Dunia. Angeshiriki, angesikia msimamo wa Rais wake kuhusu RC Makonda, na angekuwa na mawili tu ya kuchagua, kumuunga mkono Rais wake au kujiuzuru.
Nayaona manne makubwa:
1. Kutofautiana kwa Nape na Makonda katika suala la Wema kutajwa kwenye orodha hadi kufikia kupigana vijembe kumekuwa na athari kubwa. Hakuna dhambi ya kutofautiana, lakini, kulikuwa hakuna maana ya kuendelea kupigana vijembe.
2. Tume ya Nape kumjumuisha mhariri ( Balile) ambaye gazeti analoliongoza lilibeba habari dhidi ya Makonda katika siku hiyo hiyo ya kutajwa kwa Kamati na ni mhariri huyo huyo ndiye aliyesoma ripoti. Hilo lilikuwa na walakini mkubwa.
3. Umoja wa ghafla wa watu wasiopikika chungu kimoja kutaka Makonda atumbuliwe ( Rejea goli la mkono). Hili linaleta mitazamo mipya kwamba huenda suala zima lina siasa ndani yake. Kwa pamoja inajengeka dhana ambayo haipaswi kupuuzwa, kuwa zoezi zima lilichukuliwa kwa maslahi binafsi zaidi kuliko linavyoelezwa hadharani. Ni kweli, na tumesikitishwa sana na kitendo cha RC Makonda alichofanya pale Clouds TV.
RC Makonda alilikoroga na alistahili Kukemewa, lakini, hiyo usitutie upofu kushindwa kuyaona mashimo kwenye mchakato wa kushuhulika na mapungufu ya RC Makonda. Mchakato usiwe uliojaa mashaka, na mashaka haya huondolewa kwa wenye kuyashuhulikia kutanguliza weledi na kuweka kando yasiyohusika.
Hata tunapozungumzia dhana ya kugomea habari za RC Makonda si sahihi. Kimsingi tunaweza kugomea habari za Makonda lakini si RC Makonda. Habari za RC Makonda ni habari zenye kuhusu Serikali na Wananchi. Habari za Makonda kama Makonda, iwe amekwenda kucheza muziki au harusini hizo zinabaki kuwa habari za Makonda.
4. Hili la nne ndio kosa kubwa alilofanya Nape; Kuendelea na zoezi lake hata baada ya Rais 'kufunga mjadala'. Kama Waziri wa Habari, Nape ni Msemaji Mkuu wa Serikali inayoongozwa na aliye madarakani. Katika kazi hiyo, na kwenye Jamhuri, wakati mwingine Waziri wa Habari husema ' Kama kasuku' , kile kilichosemwa na Rais, hata kama ukikaa naye pembeni anaweza kukwambia kuwa hakubaliani nacho.
Hitimisho, uamuzi wa kumtoa Nape kwenye Baraza ni sahihi ili kurudisha nidhamu na mtiririko mzuri wa utendaji kiserikali.
Nape Nnauye ameshindwa kuendana na midundo au kusaidia kupanga midundo ya kwenda pamoja na aliye juu kwenye Jamhuri na Serikali kwa ujumla.
Katika wakati nchi iko kwenye utekelezaji wa miradi mingi midogo na mikubwa huku ikikopa kugharamia hayo. Ni mikopo ya Watanzania kuilipa, si ya Magufuli. Inahitajika hamasa kubwa ya kuwafanya Watanzania wafanye kazi. Waziri wa Habari ni mmoja wa watu wa kuifanya kazi hiyo.
Ni imani yangu, kuwa Nape ni kijana, mahiri na mwenye ushawishi mkubwa. Anahitaji kutulia na kutafakari namna atakavyoweza kuisaidia Chama chake na nchi kwa nyakati zijazo.
Maggid Mjengwa.