NEWS

27 Februari 2018

DARASSA KAZIMA, KAPOTEA AU KAPUMZIKA?

Maisha na muziki, acha maneno weka muziki,

Ukiwa sad ukiwa happy,

Ukiwa juu ukiwa chini piga muziki,

(Yeeeeah)

Safari na muziki, acha maneno weka muziki,

(Yeeeah)

Kila unachopenda na ukitaka kucheza cheza muziki…

UKIKUMBUKA mistari hii unaweza kujiuliza maswali mengi juu ya alipo kwa sasa staa huyu kwani alisumbua vilivyo na ngoma hii ya Muziki iliyogeuka na kuwa wimbo wa Taifa kwa kipindi kifupi.

 

DARASSA NI NANI?

Kwenye gamba lake la kuzaliwa anatambulika kama Sharif Thabeet lakini kisanii ni Darassa, maskani yake kubwa ni Kiwalani jijini Dar ambapo ndipo chimbuko lake la Muziki wa Bongo Fleva hasa lilipoanzia.

Nimeanza kumjua Darassa kitambo kidogo japokuwa rasmi kwenye gemu la Bongo Fleva alianza kutambulika 2013 alipotoa Wimbo wa Weka Ngoma chini ya Prodyuza Tuddy Thomas akiwa amemshirikisha mkali mwenzake aliyekuwa akiunda Kundi la La Familia wakati huo, Lameck Ditto.

 

Ukiachana na utambulisho wa Weka Ngoma kisha baada ya miaka miwili akaachia Sikati Tamaa akimshirikisha Ben Pol, Darassa ni miongoni mwa wakali wanaosifiwa kwa uandishi mzuri wa mashairi na kuthibitisha hilo jaribu kusikiliza nyimbo Kama Utanipenda akimshirikisha Rich Mavoko, Kaa Tayari akishirikishwa na R.O.M.A Mkatoliki, Sio Mbaya, Tunaishi, Utanitoa Roho na Muziki utaelewa namaanisha nini.

 

SIRI YA MUZIKI WAKE

Ukiachana na kutoa ngoma zenye mashairi ya kuvutia, moja ya siri alizowahi kuniambia Darassa, ni mtu mmoja poa kwa kila mtu, anaonesha nidhamu hata kwa mtu asiyemjua na pia huwa anamuamini kila anayefanya naye kazi.

 

Mfano mzuri ni pale alipokutana na Prodyuza Abbah kwa mara ya kwanza ambapo alikuwa na Mavoko wakielekea studio nyingine kurekodi lakini gari ya Mavoko ikaharibika njiani karibu na studio za Abbah ndipo walipopitia kuangalia mazingira na kujikuta wakirekodi hapohapo Ngoma ya Kama Utanipenda na baada ya hapo akamrudia tena Abbah kufanya naye Ngoma ya Muziki.

KUPOTEA KWAKE

Kwa miaka mitatu mfululizo Darassa alikuwa akiachia ngoma zilizotikisa soko la Bongo Fleva, alianza na Kama Utanipenda, Siyo Mbaya, Too Much, Muziki na Hasara Roho na zote zilitokea kuteka nyoyo za mashabiki wengi na wengine kumuona kama mfalme mpya wa Bongo Fleva.

 

Ikumbukwe pia, ndani ya miezi tisa ngoma yake ya Muziki ilifikisha watazamaji zaidi ya milioni 10 katika Mtandao wa Youtube jambo ambalo halijawahi kutokea kwa mwanamuziki yeyote wa Hip Hop Bongo.

 

Ni mwaka sasa unaenda kukatika tangu mara ya mwisho atoe Ngoma ya Hasara Roho, Mei mwaka jana. Si kwenye ‘interview’ au kitaani, Darassa amekuwa hapatikaniki. Mashabiki wengi bado wana viulizo juu ya alipo na hatma ya muziki wake ukizingatia alikuwa ameshaanza kuliteka soko.

 

SIRI YA KUPOTEA IPI?

Siwezi kumuombea mabaya lakini, wapo mastaa wengi kwenye tasnia hii ya Bongo Fleva ambao walikuwa juu sana kwenye gemu ya Bongo Fleva lakini ghafla wakapotea na hata walipoibuka wengine walikuwa wameshatumbukia katika matumizi mabaya ya madawa ya kulevya.

 

Mfano mzuri ni wanamuziki kama Lord Eyez, Chid Benz na Ray C ambao walikuwa wakifanya vizuri kwenye muziki hakuna aliyebisha uwezo wao kwani kila mmoja alikuwa ameshatengeneza mashabiki lukuki lakini walikuja kupotea na walipoibuka tayari walikuwa wameathiriwa na madawa ya kulevya.

 

Bongo Fleva ya sasa imebadilika, ukiachia ngoma ni vyema ukaendelea kusikika kwenye redio, TV, mitandao kupitia interviews pamoja na shoo ili mashabiki waendelee kuwa karibu.

 

Ushauri wangu wa bure kwa Darassa ni kuona akiachia ngoma mpya, kuibuka kwa mashabiki kupitia interviews za redio na TV na hata kuwa karibu na mitandao kuliko kuendelea kukaa kimya ambako kunawafanya baadhi ya mashabiki wajiulize kama kaamua kupumzika, kazima au kapotea!

 Makala: Andrew Carlos | UWAZI

The post DARASSA KAZIMA, KAPOTEA AU KAPUMZIKA? appeared first on Global Publishers.