KWA wafuatiliaji wa masuala ya burudani, mtakumbuka kwamba mwishoni mwa mwaka 2013, msimu wa sikukuu za Krisimasi na Mwaka Mpya, msanii Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, kipindi hicho akiwa anatamba na wimbo wake wa My Number One, alifanya mashindano ya kucheza muziki kwa watoto, aliyoyapa jina la Ngololo Dance Challenge.
Mashindano yalifanyika katika Viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo watoto kutoka kona mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam walitoana jasho kucheza na kuimba kibwagizo cha Ngololo kilichokuwa ndani ya wimbo wake wa My Number One, ambao kwa kipindi hicho ulikuwa moto kwelikweli.
Ahadi aliyoitoa, ni kwamba washindi wa shindano hilo, watakula shavu la nguvu la kusomeshwa kwenye shule nzuri (International Schools) ambapo nguli huyo wa Bongo Fleva angewagharamia kwa kila kitu mpaka watakapohitimu darasa la saba.
Watoto wengi walijitokeza lakini wawili kati yao, Hamis Fadhil na Hilal Saleh walionekana kutisha Zaidi kwa kuimba na kucheza ngololo vilevile kama msanii huyo alivyokuwa akicheza kwenye Video ya My Number One.
Kwa bahati nzuri, baada ya washindi hao kupatikana, kama mwenyewe alivyoahidi, Diamond aliwahamisha shule za ‘kayumba’ walizokuwa wakisoma na kuwapeleka East Africa International School iliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, ikadaiwa eti AMEWALIPIA ada ya mwaka mzima, kila mtu akampongeza kwa alichokifanya.
Miaka ikazidi kuyoyoma, baadaye zikaanza kuvuma tetesi kwamba Diamond amewakacha watoto hao, hawalipii tena ada kama alivyoahidi na kwamba walikuwa wakirudishwa nyumbani kwa sababu ya karo, baadhi ya vyombo vya habari vikapaza sauti, baadaye suala hilo likazimwa kimyakimya.
Yote tisa, kumi ni tukio lililotokea juzikati na kuripotiwa kwa ukubwa na gazeti hili, toleo lililopita ambapo mmoja kati ya watoto wawili waliokuwa wakisomeshwa na Diamond, Hamis Fadhil, aliibuka upya na madai kwamba ametelekezwa na Diamond na kwamba amesimamishwa masomo kwenye shule aliyopelekwa na msanii huyo kwa sababu ya kudaiwa ‘mamilioni’ ya ada.
Kama ushahidi, Hamis ambaye alipaswa kuwa darasa la saba mwaka huu (2018), alikuja na barua ambayo kweli ilikuwa ikionesha kwamba
Amesimamishwa masomo kutokana na kuwa na deni kubwa kwenye ada!
Waandishi wa habari hiyo walipomuuliza ni kiasi gani alikuwa akidaiwa, Hamis alisema hajui lakini kwa mujibu wa mwalimu mkuu wa shule hiyo, Methali Mahiri, mtoto huyo alikuwa akidaiwa shilingi milioni 12, na kwamba hakulipiwa karo hata mara moja tangu alipofi kishwa shuleni hapo mwaka 2014.
Taarifa zaidi zinaeleza kwamba uongozi wa shule umeamua kuchukua uamuzi huo, baada ya kuona kwamba kuna ubabaishaji mkubwa kwenye malipo ya ada za watoto wote wawili waliofi kishwa na Diamond shuleni hapo, na kwamba Hilal, naye hakuwa amelipiwa hata senti tano hadi alipohitimu darasa la saba mwaka jana!
Achana na visingizio vyote vinavyotolewa na Diamond na menejimenti yake, kilicho wazi kwenye sakata hili ni kwamba kumbe tangu awafi kishe shuleni hapo, Diamond HAJAWALIPIA ada kama alivyoahidi!
Amewatelekeza! Amewadanganya watoto, amewadanganya walimu, amewadanganya wazazi na walezi na amewadanganya Watanzania wote.
Kuweka rekodi sawa, siku Diamond alipowapeleka watoto hao kwenye shule hiyo, alipiga picha na kuziposti mitandaoni na zikaruka pia kwenye vyombo vya habari, zikiwa na maelezo kwamba ameshawalipia zaidi ya shilingi milioni sita na laki saba kwa wote wawili! Ingia mitandaoni utaona ushahidi wa hiki ninachokisema.
Sasa unajaribu kujiuliza, msanii mkubwa kama Diamond, kufanya mambo ya hovyo kiasi hiki, anategemea jamii inajifunza nini kutoka
kwake? Mbaya zaidi, aliwatoa watoto kwenye shule za serikali ambazo kwa sasa hakuna malipo, amewapeleka huki akitaka misifa na mwisho amewaacha kwenye mataa, afadhali yule mwingine aliyehitimu darasa la saba kimungumungu, vipi kuhusu Hamis?
Diamond anategemea jamii itaendelea kumheshimu na kumuunga mkono ikiwa anajiona ni mjanja kuliko Watanzania wote?
Sikiliza kijana, hakuna mtu aliyekulazimisha kuwasomesha watoto hao!
Ni wewe mwenyewe ndiye uliyewapandisha jukwaani, ukawachezesha ngololo na kuahidi kuwasomesha! Hakuna aliyekulazimisha!
Ukishatoa ahadi, hata kama ni kwa hiyari yako, inakuwa deni. Una deni, tena deni kubwa kwa sababu linagusa moja kwa moja maisha ya watoto hawa wawili.
Kama ulifanya yote yale kwa msukumo wa upendo kutoka ndani ya moyo wako, TIMIZA ulichokiahidi lakini kama ulifanya ili upate MISIFA huku ukijua kwamba huna nia, umewakosea sana Watanzania na ipo siku watakuadhibu. Tace care!
Hashim Aziz | Za Chembe Lazima Ukae
The post Diamod Tekeleza Ulichokiahidi, Acha Ubabaishaji appeared first on Global Publishers.