NEWS

27 Februari 2018

Muhimbili Wafanya Upasuaji Maalumu wa Mgongo

Muhimbili Wafanya Upasuaji Maalumu wa Mgongo

Madaktari bingwa wa Taasisi ya Tiba Mifupa Muhimbili (Moi) kwa kushirikiana na madaktari wa Hospitali ya BLK India leo wamefanya upasuaji maalumu wa mgongo kwa kutumia matundu (minimal invasive spine surgery) kwa mgonjwa aliyedhoofika uti wa mgongo.

Upasuaji huu umefanywa kwa mafanikio na jopo la madaktari bingwa wanne ambao wameongozwa na Daktari bingwa wa upasuaji wa mgongo, Profesa Joseph Kahamba wa Moi na mtaalamu wa upasuaji wa mgongo kwa njia ya matundu, Dk Puneet Girdhan kutoka hospitali BLK India ambapo wamekamilisha upasuaji huo kwa saa nne.

Akizungumza wakati wa upasuaji huo, Profesa Kahamba amesema unamwezesha mgonjwa kupona kwa muda mfupi, kutopata jeraha kubwa la mgongo na kutoongezewa damu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moi, Dk Respicius Boniface amesema wao na Hospitali ya BLK ya India walianzisha ushirikiano mwaka 2016 na hii ni mara ya pili kwa wataalamu kutoka hospitali hizo kufanya upasuaji kwa kushirikiana.

"Pamoja na upasuaji huu, tumeanzisha huduma za upasuaji wa magoti kwa njia ya matundu (athroscopy) ambapo tayari zaidi ya wagonjwa 300 wameshafanyiwa kwa ufanisi mkubwa na wagonjwa wengine wengi wanaendelea kunufaika zaidi," amesema.

Amesema kutokana na mabadiliko ya teknolojia ya matibabu , upasuaji wa kupanua njia za mishipa ya fahamu na kuimarisha uti wa mgongo kwa nyenzo za kisasa umeshika hatamu na Moi inafanya mabadiliko makubwa ili kuendana na teknolojia mamboleo kutoa huduma.