WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Alphonce Sebukoto, na kuagiza achungunzwe na vyombo husika.
Amechukua hatua hiyo baada mwanasheria huyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kushindwa kuishauri vyema halmashauri hiyo na kuisababishia hasara ya sh. milioni 279.
Majaliwa amemsimamisha kazi Sebukoto leo wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa halmashauri hiyo akiwa katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
“Mwanasheria utasimama kazi kuanzia leo na tuhuma zako zitachunguzwa kikamilifu na vyombo husika na uchunguzi ukibaini kama huna kosa utarudi kazini. Hatutakuonea lakini hatuwezi kukuvumilia kwa utaratibu huo ulioufanya,” alisema Majaliwa.
Amesema mwanasheria huyo Novemba 2017 wakati alipokuwa anakaimu nafasi ya ukurugenzi aliidhinisha malipo ya sh. milioni 279 zilipwe katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Anthony Bahebe.
Waziri Mkuu aliongeza kwamba Bahebe aliishtaki halmashauri hiyo akidai kulipwa fedha kwa ajili ya kazi ya ukandarasi wa mradi wa maji Igenge uliojengwa na kampuni ya ukandarasi ya Seekevim ambapo alisema mradi huo ulianza 2014 na ulitakiwa ukamilike 2015. Mwanasheria huyo aliidhinisha malipo hayo wakati ambao tayari hati maalumu ya uwakilishi ilikuwa imekwisha tangu Desemba 2015.
“Mwanasheria amemlipa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kufanya kazi na Halmashauri baada ya kuifikisha Halmashauri yake Mahakamani. Amemlipa fedha wakati kazi yenyewe ilikuwa haijaisha na aliharakisha malipo hayo kipindi ambacho Mkurugenzi hayupo, ” aliongeza Majaliwa ambaye aliwakumbusha watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utumishi na matakwa ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema fedha alizolipwa Bahebe zingeweza kutumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo.
Awali, Waziri Mkuu alifungua mabweni ya watoto wenye mahitaji maalumu katika shule ya msingi ya Mitindo iliyoko wilayani Misungwi na kisha alikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
The post MWANASHERIA ATUHUMIWA KUSABABISHA HASARA YA MIL 279 appeared first on Global Publishers.