
VIONGOZI wanne kati ya saba wa Chama cha Demokrasia na Maendelo (Chadema) walioitwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, wamefika leo katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar (Sentro) kwa ajili ya kuhojiwa kutokana na tuhuma zinazowakabili.
Viongozi hao waliowasili ni Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Mnyika (Mb), Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, John Heche; Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Halima Mdee ambaye alidai amewasindikiza wenzake na Ester Matiko ambaye ni mweka hazina wa Bawacha.
Akizungumza na wanahabari mara baada ya kutoka katika ofisi za Mambosasa, Mnyika alisema hawakuhojiwa na badala yake wameambiwa warudi tena kituoni hapo Alhamisi ijayo, Feb. 27, saa 4:00 asubuhi kwa ajili ya kuhojiwa.
Aidha, Mnyika amesema viongozi wengine hawakuweza kufika kwa sababu wapo mbali na Dar huku Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Mashinji akiwa safarini nchini Marekani.
Wengine walioitwa na Mambosasa na hawakupata nafasi ya kufika leo ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji na Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu.
Jana, Mambosasa alieleza kuwa viongozi hao ni watuhumiwa na kama wameitwa polisi ni fadhila tu, ila kwa yaliyotokea wanapaswa kukamatwa.
Wito wa viongozi hao polisi umekuja siku siku nne tangu kutokea kwa kifo cha Akwilina Akwilini, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) aliyeuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiandamana kuelekea ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao.
Na Edwin Lindege | GPL
The post Viongozi Wanne Chadema Wafika Sentro Kuhojiwa appeared first on Global Publishers.