Viongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo wakiongozwa na Zitto Kabwe wameanza ziara katika mikoa minane kutembelea kata ambazo zinaongozwa na chama hicho.
Taarifa kwa umma, iliyotolewa leo Jumatatu Februari 19, 2018 na Zitto, imesema katika ziara hiyo ameambatana na mwenyekiti wa kamati ya chama hicho inayoshughulia Bunge na Serikali za Mitaa, Annamarrystella Mallack, katibu wa kamati hiyo, Janeth Rithe na mwenyekiti wa Kamati ya Sera na Utafiti, Emmanuel Mvula.
Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini amesema: “Tumeanza ziara ya mikoa minane kutembelea kata mbalimbali ambazo wananchi walichagua madiwani kutoka chama chetu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.”
“Ziara itafanyika kwa siku 19 katika mikoa minane husika, ambako leo (Februari 19,2018) tumeanzia Kata ya Kiparang’anda, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.”
Amesema lengo la ziara ni kuwashukuru wananchi, kushiriki kazi za maendeleo katika kata, kuzungumza na kamati ya maendeleo ya kata, kuzungumza na wananchi husika, kuangalia utendaji wa madiwani kutokana na matarajio ya wananchi, kuona vikwazo na changamoto za madiwani wao.
Pia, amesema watasisitiza uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi kwenye masuala yote ya kata, pamoja na kufanya tafiti juu ya masuala ya kisera na miradi ya maendeleo ambayo ACT Wazalendo Taifa wanaweza kuyabeba kusaidia madiwani.