HAONDOKI! Hii ni kauli ya Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa raia wa Afrika Kusini alipoulizwa kuhusiana na kuondoka kwa mshambuliaji wa timu hiyo, Meddie Kagere.
Mazingisa ametoa kauli hiyo baada ya kuulizwa kuwa endapo Simba itakuwa tayari kumuachia nyota huyo kwa dau la shilingi bilioni moja kwa timu za Azam FC au Yanga.
Ikumbukwe Kagere amewahi kuhusishwa kutakiwa na klabu kubwa za Afrika zikiwemo nchi za Misri na Algeria, hii ni baada ya kuonyesha kiwango kikubwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita akiwa na Klabu ya Simba.
Kagere ambaye alifanikiwa kufunga mabao sita katika Ligi ya Mabingwa msimu uliopita na 23 katika Ligi Kuu Bara, amekuwa akiwindwa na timu nyingi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kucheka na nyavu.
Akizungumza katika mahojiano maalum na waandishi wa Championi, jana, alipotembelea ofisi za gazeti hili zilizopo Sinza Mori, Dar, Mazingisa alisema kuwa ni suala gumu kwao kukubali kumuachia mshambuliaji huyo kutokana na mchango wake kwenye timu hiyo.
“Binafsi siwezi kukubali kumuachia aondoke hata kwa bilioni moja kwa sababu najua umuhimu wa mchezaji mwenyewe kwetu, sasa unawezaje kukubali kumuachia.
“Unajua yule ni mchezaji muhimu kutokana na mchango wake kwenye timu, lakini pia amekuwa akiburudisha na timu kupata matokeo, sasa leo unaanzaje kukubali kumuachia, si unataka mashabiki waje uwanjani na mabango ya kutaka CEO aondoke.
“Mchezo wa soka ni biashara lakini ambacho unatakiwa kufahamu ni wakati gani ambao unaweza kufanya kitu kwa ajili ya timu na siyo ilimradi kufanya tu kwa kuwa ni kazi.
“Kwa Simba sasa huwezi kumuuza Kagere kwa kuwa ndiye mchezaji muhimu na bora sana na hakuna aliye tayari kuziba pengo lake kwa wakati huu,” alisema Mazingisa.
Kagere ni mchezaji muhimu Simba ambapo alijiunga nayo msimu uliopita akitokea Gor Mahia ya Kenya na msimu wake wa kwanza alifanikiwa kumaliza akiwa amefunga mabao 23 na kuwa mfungaji bora pamoja na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Ibrahim Mussa na Martha Mboma
The post Kisa Yanga… Simba Yakataa Bilioni 1 Ya Kagere appeared first on Global Publishers.