NEWS

16 Novemba 2019

Taifa Stars Yaichapa 2-1 Equatorial Guinea michuano ya Kufuzu Afcon 2021.

Taifa stars jana imeanza vema michuano ya Afcon kwa kuibuka kidedea mbele ya timu ya Equatorial Guinea kwa kupata ushindi wa mabao 2-1 mchezo uliochezwa uwanja wa Taifa.

Stars iliyo chini ya Etienne Ndayiragije iliyoanza kwa kasi kipindi cha kwanza haikuweza kutumia vema nafasi saba za kipindi cha kwanza na kuruhusu wapinzani wao Equatorial Guinea kuandika bao la kwanza dakika ya 15 kupitia kwa Pedro Obiang akimtungua kipa mkongwe wa Tanzania, Juma Kaseja kwa shuti la mbali.

Dakika tano baada ya kuanza kipindi cha pili, kocha Mrundi wa Tanzania, Etienne Ndayiragijje alianza na mabadiliko ya kuongeza nguvu katika safu ys ushambuliaji, akimtoa beki wa kulia Hassan Ramadhani Kessy na kumuingiza mshambuliaji, Ditram Nchimbi.
 
Ni mabadiliko hayo yaliyoisaidia Taifa Stars kupata bao la kusawazisha likifungwa na kiungo mshambuliaji wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Simon Happygod Msuva dakika ya 68 akimalizia mpira uliookolewa na kipa baaada ya yeye mwenyewe kuunganisha kwa kichwa kona ya beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
 
Taifa Stars iliongeza kasi ya mashambulizi baada ya bao hilo na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 90  baada ya kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar Junior ‘Sure Boy’ kufunga bao la ushindi kwa shuti la mbali.
 
Baada ya ushindi huo, Taifa Stars itasafiri kuwafuata Libya Uwanja wa Mustapha Ben Jannet mjini Monastir Jumanne ya Novemba 19 kwa mchezo wa pili wa kundi hilo.