
MSANII wa Bongo Fleva, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ amehukumiwa kulipa faini ya Tsh. Milioni 14 na mahakama ya Mwanzo wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam baada ya kupatikana na hatia ya utapeli.

Katika kesi hiyo iliyotolewa hukumu leo Machi 1, 2018, imethibitika kuwa Shilole alichukua kiasi cha Tsh. Milioni tatu kwa Mary Musa kwa ajili ya kufanya shoo siku ya mkesha wa Pasaka mwaka jana 2017 katika Ukumbi wa Heinken uliopo Mbagala-Kijichi jijini Dar es Salaam na kushindwa kufika kwa muda waliokubaliana.

Kufuatia kitendo hicho, mashabiki waliofika walifanya vurugu na kumsababishia mwandaaji wa shoo hiyo (Mary) hasara ya Tsh. Milioni 14 ambazo mahakama imeamua Shilole azilipe haraka iwezekanavyo.

Akisoma hukumu hiyo, hakimu wa mahakama ya Mwanzo Kinondoni, A. P. Mshingwa amesema Shilole amekuwa akitumiwa wito mara kwa mara na mahakama afike kusikiliza kesi yake lakini amekuwa akikaidi kufanya hivyo hadi mahakama ilipomuandikia wito mwingine kwenye Gazeti la Uhuru lakini hakufika pia.

Mahakama imemuamuru azilipe pesa hizo haraka ndani ya wiki moja vinginevyo mali zake zitaanza kukamatwa.

Shilole aliambatana mahakamani hapo na mumewe, Ushebe, na wakili wake ambaye baada ya kufuatwa kwa mahojiano na Global TV, alikataa kutaja jina lake wala kuzungumza chochote kuhusu kesi hiyo.

The post Breaking News: Shilole Ahukumiwa kwa Utapeli na Kusababisha Hasara appeared first on Global Publishers.