NEWS

18 Agosti 2018

ATCL Kuanza Kupasua Anga la Entebe Uganda na Bujumbura

Shirika  la Ndege nchini (ATCL) litaanza kufanya safari za kwenda Entebbe, Uganda na Bujumbura, Burundi kuanzia mwishoni mwa mwezi huu. Kuanza kwa safari hizo ni jitihada za shirika hilo kujitanua kibiashara baada ya kuendelea kufanya vyema katika soko la ndani.

Ndege zitakazofanya safari hizo ni Bombardier Dash 8 Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja.

Mkurugenzi Mtendaji na Mtendaji Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi, amesema kuwa safari ya kwenda Entebbe zitaanza Agosti 26, wakati safari za kwenda Bujumbura zitaanza Agosti 30, mwaka huu.

Akifafanua zaidi kuhusu safari hizo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa ATCL, Josephat Kagirwa, alisema kuwa safari hizo zitakuwa zikifanyika mara tatu kwa wiki.

Kwa mujibu wa Kagirwa, safari za kutoka Dar es Salaam kupitia Kilimanjaro kwenda Entebbe zitakuwa zikifanyika siku za Jumanne, Ijumaa na Jumapili, wakati safari za kutoka Dar es Salaam kupitia Kigoma kwenda Bujumbura zitakuwa zikifanyika siku za Jumatatu, Jumatano na Jumapili.

“Ndege zote mbili zitakuwa zikianza safari zake kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam saa 3:30 asubuhi, lakini ndege inayoenda Entebbe itakuwa ikirejea Dar es Salaam saa 8:50 mchana na ile inayoenda Bujumbura itakuwa ikirejea Dar es Salaam saa 10 jioni,”alieleza Kagirwa.

Kagirwa aliongeza kuwa kwenye kila ndege kutakuwa na daraja la biashara na daraja la kawaida ambapo kwenye daraja la biashara kutakuwa na viti sita na viti vingine 70 vilivyosalia ni kwa ajili ya daraja la kawaida.

Alisema kuwa ATCL imeweka bei nafuu kwa wateja wao watakaokuwa wakisafiri na ndege hizo kwenda Entebbe na Bujumbura, lakini pia utaratibu wa kupata tiketi ni ule ule wa ama kufika kwenye ofisi za ATCL, kukata kwa njia ya mtandao au kupitia kwa mawakala wao.

Kwa mujibu wa Kagirwa, pamoja na kutoa huduma, lakini lengo za kuanzishwa kwa safari hizo ni kukuza biashara na utalii nchini.