NEWS

29 Novemba 2019

Malipo ya Korosho yatajwa kuchochea Biashara ya Ngono


Malipo ya Korosho kwa wakulima wilayani Masasi Mkoani Mtwara yametajwa kuwa ni chanzo cha ongezeko la uwepo wa kina dada wanaofanya biashara ya ngono wilayani humo ili kujipatia fedha hizo za korosho.

 Hayo yalisemwa  jana wilayani Masasi na Madiwani wa halmashauri ya mji Masasi walipokuwa wakizungumza  kwa nyakati tofauti kwenye kikao cha baraza la Madiwani.

 Walisema katika wilaya ya Masasi hivi sasa kumekuwa na makundi mbalimbali ya wasichana kutoka maeneo mbalimbali ya mikoa ya Tanzania ambao wanafanya biashara ya ngono.

Diwani wa kata ya Mkuti, Hamza Machuma alisema kata yake ya Mkuti kuna makundi ya wasichana ambao wamekodi vyumba mitaani na biashara yao kubwa ni biashara ya ngono.

Alisema wasichana hawa mara nyingi wamekuwa wakionekana hasa katika kipindi cha misimu ya mauzo ya zao la korosho kwa vile wanafahamu kipindi hiki wakulima wanapata fedha za zao hilo.

"Tunaomba hatua zichukuliwe dhidi ya makundi haya kwani biashara inayofanyika na hawa wadada sio rasmi," alisema Machuma

 Naye diwani wa kata ya Mkomaindo, Ally Salvatory alisema halmashauri isisite kuchukua hatua ili kuwanusuru wakulima wasipoteze fedha zao.

Madiwani wa Halmashauri ya mji Masasi wakifuatilia jambo.

 Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa jimbo la Masasi, Rashidi Chuachua alisema kwa kasi ya wasichana kutoka maeneo mbalimbali kuja Masasi kwa ajili ya kufanyashughuli ya biashara ya ngono ni kubwa na lazima idhibitiwe.

"Tumeona maeneo mbalimbali hapa nchini wasichana kama hawa ambao wanafanyabiashara hii ambayo sio rasmi wakichukuliwa hatua na sisi hapa kwetu tusifumbie macho," alisema Chuachua

Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya mji Masasi, Gimbana Ntavyo alisema awali wataalamu wa halmashauri hiyo wamekuwa wakiwatembelea kwenye maeneo na kuwapa elimu mbalimbali ikiwemo ya ujasiliamali.

Alisema lengo kuwapa elimu ya masuala ya ujasiliamali na afya ni  kuona  wanaachana na shughuli hiyo badala yake watafute shughuli zingine za kihalali na waweze kujipatia kipato.