NEWS

29 Novemba 2019

Mbowe awakwamisha wanaompelekea fomu ya Uenyekiti


Baadhi ya Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), waliomchukulia fomu ya kutetea kiti chake cha Uenyekiti, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, hadi sasa wamekwama kumkabidhi fomu hiyo kulingana na hali yake ya kiafya kutokuwa imara.


Akizungumza leo Novemba 29, 2019 na EATV& EA Radio Digital, Mratibu wa zoezi la kumchukulia fomu Mwenyekiti huyo, kutoka kanda ya Dar es Salaam, Twaha Mwaipaya, amesema kuwa licha ya afya ya Mbowe kutokuwa imara, lakini wao kama vijana hawajakata tamaa na kwamba watahakikisha wanampelekea ili aijaze na kesho Novemba 30, aweze kuirejesha kabla ya 10: 00 jioni.

"Mpaka sasa Mbowe hajakabidhiwa fomu, tulipanga tumpelekee siku ya Jumatano lakini tulishindwa kutokana na afya yake kutokuwa nzuri, kesho ndiyo siku ya mwisho ya kurudisha fomu, tunafanya juhudi za hapa na pale ili tumfikishie na yeye aijaze na kuirudisha na aweze kugombea hiyo nafasi, maana ni haki yake ya msingi na ninaamini sisi kama vijana tutafanikiwa" amesema Mwaipaya.

Siku ya Novemba 25, 2019, baadhi ya Vijana wa chama hicho kutoka maeneo mbalimbali walijitokeza kwa wingi, Ofisi za Makao Makuu ya chama hicho, yaliyopo Mtaa wa Ufipa Kinondoni, Dar es Salaam, kuchukua fomu kwa ajili ya kumshawishi Mbowe kuendelea kushikilia nafasi hiyo kwa kile walichokieleza kuwa, Mbowe ni kiongozi shupavu na ni mwamba usiotikisika.