NEWS

23 Agosti 2018

BREAKING: Bobi Wine Akamatwa Upya Baada ya Kuondolewa Mashtaka Uganda

Mbunge wa Kyadondo nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine amekamatwa muda mfupi baada ya mahakama ya kijeshi kumuondolea mashtaka ya umiliki haramu wa silaha nchini.

 

Muda mfupi baada ya kuachiliwa huru, Wine alikamatwa tena na inaarifiwa kwamba anatarajiwa kushtakiwa katika mahakama ya hakimu mkuu kujibu mashtaka ya uhaini pamoja na wabunge wengine waliokamatwa.

 

Mbunge huyo ambaye pia ni mwanamuziki nchini kwa jina maarufu Bobi Wine leo aliwasilishwa katika mahakama ya kijeshi mjini Gulu kaskazini mwa Uganda.

 

Mawakili wake awali walijuzwa kuwa kesi itasikilizwa katika kambi ya kijeshi ya Makindye anakozuiliwa mjini Kampala.

 

Kumekuwa na shinikizo kubwa kimataifa la kutaka Bobi Wine aachiwe huru.

Mawakili wa jeshi wameeleza mahakama kuwa mashtaka dhidi ya Wine yameondolewa na kwamba mwanasiasa huyo akabidhiwe kwa polisi ili akabiliwe na mashtaka ya uhaini pamoja na na wabunge wengine waliokamatwa .

 

Wakili wake Wine Medard Segona ameiambia mahakama kwamba licha ya kuwa wameridhishwa na hatua ya mahakama ya kijeshi , anapinga hatua ya sasa ya mteja wake kuhamishwa katika mahakama ya kiraia kukabiliwa na mashtaka mapya.

 

Alitaka mbunge huyo aachiwe huru ili aweze kupelekwa kupokea matibabu.

Mahakama iliamua kuwa Bobi Wine yu huru, iwapo hakuna mashtaka mengine yatakayowasilishwa dhidi yake.

 

Wakati huo Wine alionekana akilia na kupangusa machozi huku hukumu hiyo ikisomwa. Alitoka nje ya mahakama akiwa anatemba kwa magongo na kuonekana kuwa na maumivu makali.

Hapo ndipo alipokamatwa upya.

The post BREAKING: Bobi Wine Akamatwa Upya Baada ya Kuondolewa Mashtaka Uganda appeared first on Global Publishers.