ACHANA na bao alilofunga, kiungo mpya wa Simba, Hassan Dilunga ni kama amevunja ufalme wa kiungo Mzambia, Clatous Chama, kwani katika mechi mbili tu alizocheza, Dilunga ametengeneza mabao matatu wakati Chama akiwa hajatengeneza bao lolote katika mechi tatu alizocheza.
Hiyo ni ishara tosha kuwa Chama aliyejiunga na Simba akitokea Power Dinamo ya Zambia katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara kwa dola 35,000 ambazo ni karibu milioni 80 za Kibongo, ana kibarua kigumu mbele ya Dilunga aliyetua timu hiyo kwa dau la shilingi milioni 50 akitokea Mtibwa Sugar.
Awali, Chama alikuwa gumzo katika timu hiyo, ni baada ya kuonyesha kiwango kikubwa kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana.
Dilunga hadi anatua kuichezea timu hiyo hakuwa hana nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza huku Chama akiwa anaanza akicheza nafasi ya kiungo mshambuliaji namba saba.
Chama ufalme wake umevunjwa ni baada ya kuzidiwa na Dilunga ambaye yeye ameanza kucheza katika kikosi cha kwanza kwenye mechi mbili dhidi ya Arusha United ambayo alitengeneza nafasi
mbili za kufunga mabao ambayo yalifungwa na Emmanuel Okwi.
Hakuishia hapo, Dilunga alitengeneza nafasi nyingine moja kwenye mechi ya Ngao ya Jamii walipokutana na Mtibwa Sugar CCM Kirumba ambapo alimtengenezea Meddie Kagere bao la kwanza kabla ya yeye mwenyewe kufunga kwa shuti kali ndani ya 18.
Hivyo, Kocha Mkuu wa timu hiyo Mbelgiji, Patrick Aussems ana kibarua kigumu cha kuamua nani aanze katika kikosi chake hicho kutokana na viungo hao wote kuwatumia kucheza namba saba tangu aanze kukinoa kikosi hicho.
Wakati Dilunga ambaye alishindwa kuonyesha cheche zake alipokuwa Yanga misimu miwili iliyopita, akifanya vitu vizuri hivyo kwenye mechi mbili, Chama yeye ameanza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo kwa kucheza michezo mitatu ukiwemo na Asante Kotoko na mwingine mmoja aliocheza wakiwa wameweka kambi nchini Uturuki.
Akizungumzia hilo, Dilunga alisema: “Nashukuru kwanza kufanikiwa kupata nafasi ya kucheza katika timu kubwa kama Simba yenye ushindani mkubwa wa namba.
“Nisingependa kuongea sana, nimekuja Simba kufanya kazi, hivyo nitahakikisha natimiza majukumu yangu ya ndani ya uwanja, ikiwemo kutengeneza nafasi na kufunga mabao kwa kila nafasi nitakayoipata, zaidi niseme ninaomba ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzangu.”
Wilbert Molandi, Dar es Salaam.
EXCLUSIVE; DILUNGA Afunguka Namna ya Ushangiliaji Alivyoifunga MTIBWA
The post DILUNGA AVUNJA UFALME WA CHAMA SIMBA SC appeared first on Global Publishers.