KARIBU mdau wa safu hii tuendelee kupeana ‘madini’ juu ya maisha ya mapenzi. Kama mada hii inavyojieleza, si kila unapopatwa na matatizo ya uhusiano wa kimapenzi, basi ukimbilie kuomba ushauri. Mengine ni siri za ndani. Kuwa makini sana na ushauri unaopewa na mtu anayekupa ushauri huo kwani mengine ni sumu na yatakutumbukiza shimoni. Mdau usiwe mwepesi kukimbilia msaada wa ushauri au mawazo ya nini ufanye baada ya penzi lako kuingia mdudu mbaya.
Ukweli ni kwamba ukiwa muumini wa ushauri kwa kila jambo unalokutana nalo kwenye mapenzi, hicho ni kilema kibaya mno maishani mwako. Huo ni ukomo wa fikra na kuamini juu ya ushauri wa mtu kukufikisha mahali sahihi kwenye mapenzi.
Unapoingia kwenye mgogoro wa kimapenzi na mwenza wako na kukimbilia kushauriwa na mtu ambaye siyo sahihi, kwa vyovyote utaingia kwenye ‘shida’ tu. Simama kama wewe, funga mkanda kwa kuwa siyo jambo lelemama hasa linapokuja suala kubwa la uamuzi wa kuoa au kuachana na mwenza wako.
Kwenye mapenzi lazima ujipe nafasi ya kutafakari wewe kama wewe na siyo kushikiliwa akili. Kuna hasara kubwa kuliko faida kwenye suala la kuomba ushauri hasa ukizingatia ni nani uliyemuomba ushauri huo.
UTOFAUTI WA UELEWA
Wataalam wanaeleza na ndiyo ukweli halisi kwamba, kipimo cha uelewa kinatofautiana kutoka mtu mmoja kwenda mwingine. Pia utaalam au utambuzi wa mambo nao hutofautiana. Mtu anaweza kuwa mahiri katika mapishi, lakini ukimpeleka kwenye suala la mapenzi anakuwa hajui kitu, hivyo ni rahisi kukupoteza kabisa.
JIONGEZE MWENYEWE
Uchunguzi unaonesha kwamba, wapenzi wengi hupotoshwa na washauri hasa wasio wataalam wa elimu ya saikolojia na maisha juu ya tatizo au suala husika la kimapenzi. Migogoro mingine ya kimapenzi wala hahihitaji ushauri bali ni kujiongeza tu wewe mwenyewe!
KUPIMA MAMBO JUUJUU
Mara nyingi washauri hasa ambao si wataalam huwa si wao wanaokabiliana na matatizo, hivyo ni rahisi kwao kupima vitu juujuu tu na kushauri kirahisirahisi bila kufikiri juu ya madhara yatakayowapata wale wanaowashauri.
WASHAURI MAELFU
Duniani kuna washauri maelfu kwa maelfu hasa kama wewe ni muumini wa mitandao. Kwa hiyo kama utachukua ushauri kama ushauri kwa papara bila kuutathmini, basi unaweza kujikuta kwenye matatizo makubwa mno, ukitamani kurudi kule ulikotoka, lakini ikashindikana.
Fahamu kuwa, kinachotokea mara nyingi kwenye ushauri ni mtu kumfanya mwenzake awe kama yeye alivyo, yaani apuuze, aamue na apende kwa staili yake, jambo ambalo haliwezekani kabisa kwenye dunia hii ya mapenzi.
UTAFANYIA KAZI UAMUZI WA MWINGINE
Ushauri utakaopewa ndiyo utakaokuwa ukikuendesha kwa kuhofia kuwa usipoufuata utajikuta kwenye matatizo mengine au utarudi kwenye matatizo yaleyale. Huwezi kutoka nje ya mstari wa ushauri uliopewa kwani utakuwa umekosa kujiamini.
Ukiwa mtu wa kusikiliza kila ushauri unaopewa, unaweza kujikuta unachukua ushauri mwingine ambao ni sumu kabisa na matokeo yake ukajikuta ukichukua uamuzi hata wa kujinyonga au kujiua kwa sababu tu ya ushauri mbaya uliopewa na ndugu, jamaa au rafiki asiyekutakia mema.
Mwisho ni vyema kuchuja kila ushauri unaopewa na siyo kukurupuka na kuchukua uamuzi kwa sababu tu umepewa ushauri. Kwa kifupi, akili ya kuambiwa, changanya na yako! Kwa maoni, nicheki kwenye namba hiyo hapo juu. Pia tembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Ijumaa Wikienda kwenye Facebook.
The post EPUKA USHAURI HUU NI SUMU KWENYE PENZI LAKO! appeared first on Global Publishers.