STAA wa Yanga kwa sasa ni Papy Tshishimbi, hiyo ni kutokana na kucheza kwa kiwango cha juu kwa muda tangu atue kikosini hapo, lakini inavyoonekana upepo unaelekea kubadilishwa.
Hali hiyo inatokana na mazingira ya kikosi hicho wakati huu wa maandalizi ya msimu mpya wa 2018/19 ambapo mshambuliaji Mcongo, Heritier Makambo, ameonyesha uwezo mkubwa na ni matumaini kuwa atakuwa nguzo muhimu kikosini kama mambo yakiendelea hivyo.
Licha ya uwezo huo, kumekuwa na mipango kadhaa ya kiufundi kuhusu kumfanya staa huyo kuwa ‘mfalme’ kwenye suala la kutupia mabao.
Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, tayari amelifanyia kazi hiyo na amekuwa akijaribisha kombinesheni ya wachezaji wawili watakaocheza na straika huyo.
Makambo amekuwa akibadilishiwa viungo ili kuona nani na nani wanaweza kumfaa, alianza kupangwa na Faisal Salum ‘Fei Toto’ na Raphael Daudi.
Akizungumzia hilo, Zahera alisema: “Bado ninaendelea kutafuta pacha nzuri ya Makambo itakayocheza vizuri kwa kuelewana.”
Anaitaka rekodi ya Cannavaro
Mara baada ya mechi dhidi ya Kilosa Combine iliyopigwa wilayani Kilosa, nyota huyo alisema kuwa anafurahishwa na upendo wa mashabiki jambo linalomvuta kuitumikia klabu hiyo kwa muda mrefu zaidi ya Cannavaro.
“Yeye amesema kwenye maisha yake ya soka hajawahi kuona mashabiki wakarimu kama wa hapa Yanga jambo ambalo linamfanya atamani kuzeekea Yanga.
“Lakini pia amegundua ukarimu huu ndiyo ulimfanya hata Cannavaro aitumikie timu kwa muda wote wa miaka 12, kwani mapenzi yao yanatia hamasa ya kuendelea kujisikia ni mtu muhimu ndani ya klabu hiyo,” alisema mtoa taarifa.
Awafungukia Waarabu
Baada ya kuruhusiwa kucheza kwenye michuano ya kimataifa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Makambo ameweka bayana kuwa atahakikisha anafanya kitu kwenye mchezo huo wa wikiendi hii ambao watacheza na Waarabu, USM Alger kutoka Alger.
Makambo hakuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kilichochapwa mabao 3-2 dhidi ya Gor Mahia ya Kenya hivi karibuni kutokana na kuchelewa kufika kwa kibali chake ambapo kwa sasa kimetolewa na Caf.
Mshambuliaji huyo ambaye amechagua kutumia jezi namba 19, amezungumza na gazeti hili na kusema: “Ni mechi ngumu lakini sisi tunaamini kwa asilimia kubwa tutashinda.
“Ninawaomba mashabiki wajitokeze kwa ajili ya kutupa sapoti kwani wao ni muhimu zaidi na tumeona jinsi ambavyo wamekuja kwenye michezo yetu ya kirafiki walivyotupa nguvu ya kupambana na kupata matokeo.”
Kuhusu ligi kuu
“Nimesikia na kuzipata taarifa za mashabiki wa Yanga na kikubwa wanataka kuona timu yao ikipata mafanikio kupitia mimi katika kuelekea msimu ujao wa ligi.
“Niwaambie kuwa, waondoe hofu mimi nipo pamoja nao, watulie na wasubirie ligi ianze ndiyo wataona makali yangu huku nikiendelea kujifua kuhakikisha ninakuwa fiti.
“Ninajisikia furaha kuwepo kwenye timu kubwa kama hii ya Yanga yenye idadi kubwa ya mashabiki ambayo sijawahi kuiona katika maisha yangu ya soka, hivyo niwaahidi kuifanyia makubwa timu yangu mpya ya Yanga,” alisema Makambo.
Waandishi: Wilbert Molandi, Musa Mateja & Said Ally
The post Makambo Mfalme Mpya Yanga SC appeared first on Global Publishers.