MFUNGAJI bora wa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, Emmanuel Okwi, ameonekana kutaka kumshangaza kocha wake mpya wa timu hiyo, Mbelgiji, Patrick Aussems kufuatia kauli yake ya kuhusu maandalizi ya msimu ujao.
Okwi alifanikiwa kutwaa kiatu cha dhahabu msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara kwa kufunga mabao 20 akifuatiwa na John Bocco ambaye alifunga mabao 14, na dalili zinaonyesha anataka kuwashangaza wengi kwa kutetea tuzo hiyo ya ufungaji bora.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo mwenye uraia wa Uganda, anatarajia kukutana na upinzani mkubwa katika mbio za ufungaji bora msimu ujao wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuanza Agosti 22 kutokana na uwepo wa mshambuliaji wa Yanga, Mkongo, Heritier Makambo ambaye kocha wa timu hiyo, Mwinyi Zahera ameeleza kuwa ni mchezaji hatari katika kufumania nyavu.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Okwi amesema amejiandaa vizuri kwa ajili ya msimu mpya wa ligi kuu ili kuendana sawa na ushindani wa ligi kwa kujituma kuliko msimu uliopita.
“Nimejiandaa vizuri kwa ajili ya msimu mpya wa ligi kuu, nahitaji kujituma zaidi msimu ujao ili niweze kufanikiwa kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita.
“Nahitaji kuanza msimu vizuri kwa kuhakikisha nafanikiwa kufunga zaidi ya msimu uliopita, ligi itakuwa ngumu na ya ushindani, tunajipanga kuwa vizuri,” alisema Okwi.
Upande wa pili, Kocha Aussems amekuwa na matumaini na safu yake ya ushambuliaji ikiongozwa na Okwi na kudai kuwa anaamini wakiendelea kwa kasi hiyo msimu ujao watakuwa hatari zaidi.
“Kocha amefurahishwa na namna kiwango pamoja na kasi ya kufunga ya Okwi,” kilisema chanzo cha taarifa.
Alipotafutwa kocha mwenyewe alisema: “Wachezaji wote wanafanya kazi nzuri na wanatimiza vile ambavyo nimekuwa nikivitaka. Kwa sasa tunaangalia zaidi juu ya mechi yetu na Ngao ya Jamii na siyo kitu kingine.”
Stori: Khadija Mngwai na Said Ally
The post Okwi Aandaa Sapraizi Kwa Mbelgiji appeared first on Global Publishers.