NEWS

17 Agosti 2018

Tanzania Yahadharishwa Kuhusu Ugonjwa wa Ebola

Serikali  imewasisitiza Watanzania kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa ebola kwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi tisa zilizohatarini kupata ugonjwa huo.

Nchi zingine zilizotajwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa hatarini kukubwa na ugonjwa huo ni Angola, Zambia, Uganda, Malawi, Msumbiji, Burundi na Rwanda.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu hali ya ugonjwa huo, Mkurugenzi wa Ubora wa Huduma za Afya wa wizara hiyo, Dk. Mohamed Mohamed, alisema licha ya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi hizo, lakini mpaka sasa hakuna mtu aliyegundulika na ugonjwa huo. 

Alisema shirika hilo lilifanya utafiti na Tanzania imeonekana kuwa na tishio kubwa la kuingia kwa ugonjwa huo kutokana na kupakana na nchi ya Demokrasia ya Kongo.

Alieleza tangu ugonjwa huo uingie nchini Kongo hivi karibuni, watu 57 walipatwa na ugonjwa huo na kati yake 41 wameshapoteza maisha.

"Tayari tumeshaweka vituo mipakani ikiwa ni pamoja na kuweka vifaa vya kupima joto kwa wasafiri wanaoingia nchini kupitia mipakani,"alisema.

Alieleza kuwa serikali imejipanga na tayari maabara tatu zinaboreshwa katika maeneo ya Ifakara, Lindi na Temeke.

Kadhalika, alisema wameweka watalaamu katika mipaka na tayari wameshajenga kituo kikubwa Temeke ili mtu atakayehisiwa kuwa na virusi hivyo apelekwe kwa uchunguzi zaidi.

"Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kutokwa na damu ndani na nje ya mwili, kuharisha, homa kali na mwili kulegea,"alisema.

Mkurugenzi wa Msaidizi wa kitengo cha Mazingira, Dk. Khalid Massa, alisema kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa, wamekuwa wakidhibiti watu wanaoingia nchini kwa njia za panya.

Alisema wapo watumishi waliowekwa katika njia hizo na hutoa taarifa kwenye kitengo maalumu kinachoratibu hali ya ugonjwa huo wizarani.