NEWS

20 Agosti 2018

Waziri Aendesha Baiskeli Kwenda Kujifungua


Katika hali isiyokuwa ya kawaida kwa mama mjamzito, huko nchini New Zealand Waziri wa masuala ya Wanawake nchini humo, aliendesha baiskeli mwenyewe kwenda hospitali kujifungua.

Waziri huyo, Bi. Juile Genter, kutoka chama cha Kijani, amesema alimua kuendesha baiskeli kwa sababu ndani ya gari lake hakukuwa na nafasi ya kutosha ambapo alituma picha kwenye ukuraswa wake wa Instagram zikimuonesha yeye na mwenza wake wakielekea hospitali.

Bi. Genter, mwenye umri wa miaka 38, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, anafahamika kuwa mwanaharakati anayeunga mkono wananchi kutumia baiskeli badala ya magari.

Akiwa ni mzaliwa wa Marekani, Bi. Genter alitangaza ujauzito wake kupitia Instagram, akisema, “Sasa inatubidi tuongeze kiti cha ziada kwenye baiskeli zetu”.

Waziri huyo, atachukua likizo ya uzazi ya miezi mitatu akiungana na wanasiasa wengine waliojifungua watoto wakiwa bado watumishi wa umma.

Mwezi Juni mwaka huu, Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Arden, alikuwa kiongozi wa pili duniani kujifungua mtoto akingali anatumikia wadhifa wake ambapo yeye na Genter wote walijifungua katika hospitali ya umma ya Auckland City.