MKUU wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amesema anatarajia kuufanya mkoa wake kuwa kitovu cha chakula nchini na kuulisha Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza na Global TV juzi baada ya kutembelea Kampuni ya Global Group, Hapi alisema mkoa wake una bahati ya kuwa na hali ya hewa nzuri, hivyo kuwa miongoni mwa mikoa mitano inayolima kwa wingi mahindi. “Iringa ni moja ya mikoa inayozalisha mahindi, nitahakikisha kunakuwa na viwanda vingi vya kusaga nafaka ili tuwe tunasambaza unga badala ya mahindi. Lawama za mahindi kuozea kwa wakulima zisiwepo.
“Soko la unga wa mahindi lipo kwa sababu Dodoma ambako ndio makao makuu ya nchi ni karibu na Iringa kuliko Morogoro na Singida inayopakana nayo, ni karibu sana, ni kama kilomita 200 tu, hivyo tunaweza kutumia ukaribu huo kwa kupata soko la unga,” alisema Hapi.
Akizungumzia utalii, Hapi alisema Iringa ina Hifadhi ya Taifa ya Ruaha lakini haitangazwi na kuwafanya watalii kwenda kuwaona wanyama huko. “Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ni kubwa sana na ina kila wanyama lakini bado Iringa haijawa sehemu ya utalii. Nitahakikisha watalii wanakuja kwa wingi pale, ni kazi tu ifanyike kuitangaza,” alisema.
Kuhusu watumishi wa serikali alisema atahakikisha wanafanya kazi ipasavyo na kwa weledi na atahakikisha wataalamu wa kilimo, afya, elimu na kadhalika wanakuwa karibu na wananchi.“Kila mkuu wa idara atatakiwa anionyeshe kazi gani ameifanya kwa wiki, hii itasaidia kuwafanya watoke ofisini na kwenda kwa wananchi,” alisema Happi.
Katika ziara hiyo alitembezwa na Meneja Mkuu wa Global, Abdallah Mrisho sehemu mbalimbali kama vile vyumba vya habari vya magazeti pendwa ya Uwazi, Risasi, Wikienda, Amani na Ijumaa, pia alitembelea chumba cha habari cha magazeti bora ya michezo nchini, Championi na Spoti Xtra pamoja na kile cha Global TV On Line.
Aliyasifu Magazeti ya Global kwa kuwafikia Watanzania wengi hasa wale wa kawaida. “Mnafanya kazi ya ziada ndio maana magazeti yenu yanapendwa na wananchi wengi,” alisema mkuu huyo wa mkoa. Aidha, alifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji, Eric Shigongo. Mahojiano ya Happi na Global TV utaweza kuyaona ukitembelea Global TV On Line, kupitia YouTube.
Na Elvan Stambuli.
SIKU 30! RC Hapi Awasha Moto Iringa, Amtaja Msigwa, Kubenea!
The post ALLY HAPI ATAMBA IRINGA KUILISHA DODOMA appeared first on Global Publishers.