NEWS

27 Oktoba 2018

Waziri Jafo Awapiga Marufuku Wakuu wa Mikoa na Wilaya Kuwaweka Selo Madaktari

Waziri  wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amewapiga marufuku wakuu wa mikoa na wilaya kuchukua uamuzi wa kisiasa dhidi ya madaktari ikiwamo kuwaweka mahabusu.

Badala yake, Jafo amewataka viongozi hao kuunda tume maalumu za uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili. 

Jafo alipiga marufuku hiyo jana jijini Dodoma alipokuwa akifungua mkutano wa 50 wa kitaaluma wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT).

Alisema kumekuwa na mazoea ya baadhi ya viongozi wa kisiasa, hasa wakuu wa mikoa na wilaya, kuwaweka ndani watumishi wa umma wakiwamo madaktari bila kujiridhisha juu ya tuhuma dhidi yao.

"Wakuu wa mikoa na wilaya nawaagiza pale ambapo daktari anatuhumiwa kufanya kosa la aina yoyote, iundwe tume ya kuchunguza, iangalie kama kuna makosa na vyombo vya usimamizi vitimize wajibu wake badala ya kuchukua uamuzi wa kisiasa,” alisema.

Alisema madaktari wanafanya kazi kubwa ya kuokoa maisha ya watu na wakati mwingine kosa linakuwa si lao bali ni la wagonjwa wenyewe, hivyo tume ichunguze na kama ni kweli hatua stahiki zichukuliwe.

"Mimi nilishuhudia mtu tena nilimbeba kwenye gari langu mwenyewe wakati huo nikiwa meneja shirika la Plan International. Yule dada alienda zahanati na kutokana na tatizo lake, aliambiwa aende hospitali ya wilaya lakini hakwenda. Alikwenda wakati wa kujifungua, sasa kesi kama hii unaweka selo daktari wakati matatizo mengine ni ya familia," alisema Jafo.

Aidha, Jafo alisema dhamira ya serikali iliyopo sasa ni kuhakikisha inajenga hospitali katika wilaya zote ifikapo mwaka 2020.

"Kwa sasa tumeshaboresha vituo vya afya 350 na katika mwaka huu wa fedha, zimetengwa Sh. bilioni 105 kwa ajili ya kujenga hospitali 67 za Wilaya na kwa sasa ziko 77," alisema.

Naye Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Tamisemi, Dk. Ntuli Kapologwe, alisema mkutano huo umekuwa na fursa kwao ya kujadili mambo waliyotekeleza kwa mwaka uliopita na namna watakavyotekeleza kwa sasa ili kuifanya sekta hiyo iwe bora kuliko nyingine.

Alisema mikakati waliyo nayo ya kutoa sare kwa madaktari zikiwa na majina ili kukabiliana na tatizo la uwapo wa madaktari feki linaloripotiwa kutokea maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wake, Rais wa MAT, Dk. Obadiah Nyongole, alisema mkutano huo unazungumzia weledi wa kitaaluma na maendeleo ya viwanda katika kutoa huduma bora za afya kwa wote.

"Kama kaulimbiu ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, sisi wataalamu tuko tayari kushirikiana na serikali na wadau kusogeza huduma bora za afya kwa kutumia huduma ya hospitali tembezi na hilo liko kwenye mpango kazi wa MAT,"alisema.

Dk. Nyongole anatarajiwa kukabidhi mikoba ya urais wa MAT kwa Rais mpya wa 19 wa chama hicho, Dk. Elisha Osati.