Na Munir Shemweta, WANMM Kilimanjaro
Waziri wa Ardhi Nyumba na Mandeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka watendaji wa sekta ya ardhi nchini kujisahihisha ili kuepusha mogogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiwaumuzi wananchi wengi.
Lukuvi alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na wananchi 97 wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na Halmashauri ya Moshi Vijijini katika mkoa wa Kilimanjaro waliojitokeza kwa ajili ya kuwasilisha kero zao za ardhi kupitia program ya Funguka kwa Waziri.
Alisema, ni vyema katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya tano watendaji wa sekta ya ardhi wakaanza kujisahihisha ikiwemo kuweka majalada yote ya ardhi vizuri kabla hajatembelea maeneo yao kinyume chake atawashughulikia wote watakaobainika kukaidi ama kutoweka sawa majalada ya ardhi.
“Mtu yeyote anayetaka kuingusha Serikali katika masuala ya ardhi tutamuangusha yeye na lazima tutekeleze ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo” alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Serikali itawanyoosha wale wote wanaoenda kinyume na maadili ya utumishi na kubainisha kuwa hata wale watendaji wa ardhi walioharibu huko nyuma watashughulikiwa.
Akigeukia migogoro ya ardhi, Lukuvi alisema migogoro mingi inayojitokeza sasa ni ile ya miaka ya nyuma ya kuanzia miaka ya themanini na kubainisha kuwa kupungua kwa migogoro mipya kunatokana na Serikali ya sasa kuweka mazingira mazuri ya kushughulikia masuala ya ardhi.
“Leo watendaji wa sekta ya ardhi wamenyooka na kazi ya serikali ya awamu ya tano ni kuwanyoosha wale wanaoenda kinyume na taratibu na sheria katika kushughulikia masuala ya ardhi.
Akigeukia suala la wamiliki wa ardhi kuchukuliwa maeneo yao bila kulipwa fidia, Lukuvi amewahakikishia wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa, Serikali inalipa kipaumbele suala la fidia kwa wale ambao maeneo yao yatachukuliwa.
Aliwaeleza kuwa hata ikitokea mtu hakufidiwa kipindi ambacho eneo lake limechukuliwa lakini malipo yake yataanza kuhesebiwa pale eneo lilipochukuliwa na kiwango cha fidia kitakuwa kikiongezeka kadiri malipo yake yanavyochelewa.
Pia aliwaeleza wananchi waliokusanyika katika ukumbi wa ofisi wa mkoa wa Kilimanjaro kuwa wale wote ambao maeneo yao yalishatolewa maamuzi na Mahakama hakuna mtu yoyote mwenye mamlaka ya kubatilisha ikiwemo Serikali.