NEWS

1 Januari 2019

Makala: Wateule watano wa JPM ‘waliokiki’ zaidi 2018 na mambo yao


Ikiwa leo siku ya mwisho ya mwaka 2018, mwaka ambao umeshuhudia matukio mengi ya kisiasa na kiutawala nchini, umekuwa ni mwaka ambao majina kadhaa ya wateule wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli yalitajwa kwenye mijadala mingi, kwa lugha isiyo rasmi ‘yalikiki’.

Tumekuandalia orodha fupi ya majina matano ya wateule wa Rais Magufuli ambao walifanya mambo ambayo yalikuwa gumzo kwenye vyombo vya habari, mitandao ya jamii na hata mitaani.

Kangi Lugola
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola aliweka alama na kuzua gumzo kubwa baada ya kumtaka mfanyabiashara, Said Lugumi kufika ofisini kwake kutokana na mkanganyiko wa zabuni ya kufunga mfumo wa utambuzi wa alama za vidole kwenye vituo vya polisi nchini yenye thamani ya Sh37 bilioni.

Uamuzi huo wa Lugola uliamsha mijadala kutokana na umaarufu wa ‘Sakata la Lugumi’ ambalo lilikuwa linaonekana kama kisiki kilichowashinda wengi.

Ikumbukwe kuwa Lugola alikuwa mmoja kati ya wabunge waliojadili kwa undani sakata hilo bungeni mwaka 2016 na baadaye likaundiwa kamati ya watu 9 waliochunguza mkataba katia ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi.

Julai 31 mwaka huu, Waziri Lugola alikutana na Lugumi ofisini kwake, mkutano ambao ulikuwa gumzo kwenye vyombo vya habari kutokana na hatua ya aina yake aliyoichukua waziri huyo.

Baada ya mkutano huo, Lugola alisema kuwa amemsikiliza mfanyabiashara huyo na amegundua kuwa kuna mambo mengi ambayo hayajulikani kwa wengi, na kwamba pamoja na mambo mengine, Jeshi la Polisi pia lina wajibu ambao halijautekeleza ili Lugumi atekeleze mkataba husika.


Mfanyabiashara Said Lugumi (kushoto), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi , Kangi Lugola (kulia)

“Lugumi amekubali kukamilisha mradi huu, na ameomba apewe miezi minne ili ahakikishe mfumo huo anaukamilisha na kuukabidhi kwa jeshi la polisi,” alisema Lugola.

“Lakini nimemuonya kwamba kazi yangu kubwa ni kuhakikisha ile mahakama ya mafisadi… bado ina uhaba wa wateja, kwa hiyo miezi minne aliyoiomba, endapo itakamilika na yeye hajakamilisha mradi basi haraka sana atakuwa mteja wa mahakama hiyo,” aliongeza.

Aidha, Lugola alisema kuwa baada ya kumsikiliza na kupitia kwa pamoja mkataba husika, kuna baadhi ya mambo yako tofauti na ambavyo yanasemwa na kuchukuliwa na watu walio nje.

Tukio lingine lililotikisa la Kangi Lugola ni pamoja na kumtoa nje ya kikao Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza, Juma Malewa aliyechelewa takribani dakika moja kwenye kikao chake cha Julai 6 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Kamishna huyo alistaafu wiki moja baadaye.

Mengine yaliyozua mijadala ni pamoja na kuagiza polisi kutoa dhamana siku za wikendi, kuagiza kukamatwa kwa Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo Zitto Kabwe na kadhalika.



Aggrey Mwanri
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri ndiye mteule wa JPM ambaye kwa mwaka huu ametengeneza misemo ‘iliyokiki’ zaidi ikiambatana na matukio ambayo yaliwavunja mbavu watu alipokuwa katika utekelezaji wake wa kazi.

Mwanri ambaye anaonekana ni mchapakazi, ana kipaji kingine cha kushika umakini wa watu na kuwafurahisha wakati anawachoma sindano ya maagizo magumu.

Mwaka huu pekee, misemo yake mitatu imeteka vichwa vya habari, sehemu za mikusanyiko, mitandao ya kijamii na hata kutengenezea matangazo ya matamasha makubwa.

Hakuna asiyeifahamu misemo ya “Sukuma Ndani,”, “Fanya kama unajikuna”, na “Engineer Soma hiyo-Soma kwenye ramani-ngapi hiyo”. Hii ni misemo yenye ucheshi lakini ilizaliwa kwenye kazi muhimu zisiyo za ucheshi.

Mfano; kampeni ya kuwakamata watu wanaowapa ujauzito wanafunzi ilibatizwa jina la ‘Sukuma Ndani’. Onyo kwa wanaopuuzia maagizo yake au wanaoona anafanya mzaha waliambiwa wanyooshe mkono au ‘wafanye kama wanajikuna’.

Kadhalika, Mhandisi ambaye alimhisi kuwa ni ‘janjajanja’ na huenda hakuwepo kwenye eneo la ujenzi wakati wa kazi, alimpimisha vipimo kuhakikisha kama vinaendana na vilivyo kwenye ramani. Zoezi hilo lilizaa misemo ya ‘Engineer Soma hiyo n.k’. Sauti ya Mwanri yenye maneno hayo ilitumika katika tangazo la tamasha la Fiesta mwaka huu.

Ni dhahiri kuwa hotuba za Mwanri zina jumbe na ucheshi mwingi, zitakuongezea siku za kuishi kama kweli kucheka huongeza siku za kuishi. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pia alikuwa miongozi mwa waliocheka mara kadhaa alipokuwa akisikiliza hotuba ya mkuu huyo wa mkoa alipozuru mkoa huo.

Kwa watu wanaomiliki YouTube, walifaidika na video zao kuangaliwa mara nyingi zaidi walipoweka habari za ‘Mzee wa Sukuma Ndani’, ‘Fanya Kama Unajikuna’.



Mwanri alichukua nafasi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto ambaye mwaka jana msemo wake “watapata tabu sana” ulikuwa msemo wa mwaka.

Jokate Mwegelo
Julai 28 mwaka huu, jina la Jokate Mwegelo aliyewahi kushiriki mashindano ya Urimbwende (Miss Tanzania) na hata kuwa mwanamitindo maarufu, lilitikisa mitandao ya kijamii na mitaani baada ya kutajwa kuwa kati ya wateule wa Rais Magufuli. Jokate alitangazwa kuwa Mkuu wa Wilaya Mteule wa Kisarawe mkoani Pwani.

Uteuzi huu ulikutana na ukosoaji mkubwa hasa kwenye mtandao wa Twitter, vita kubwa ya maneno kati ya wakosoaji na wapongezaji iliibua mengi. Watu maarufu akiwemo Rais wa Chama Cha Wanasheria wa Tanganyika, Fatma Karume ni kati ya waliojitokeza hadharani kukosoa uteuzi huo.

Picha za zamani za Jokate akiwa kwenye maisha yake ya uanamitindo, usanii na uhusiano zilisambaa mitandaoni ghafla. Mwenyewe aliyaanza maisha mapya kwa kufuta picha zake zote kwenye Instagram, na kuanza maisha ya Ukuu wa Wilaya. Wote waliokuwa wanatumia picha zake za zamani kwa lengo la kuleta sintofahamu walipewa onyo kali na jeshi la polisi.


Kwa bahati nzuri, Jokate ambaye aliianza safari ya siasa akiwa ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), amefanikiwa kutumia changamoto hizo za kukosolewa kuonesha alichonacho ni kikubwa. Tangu ateuliwe, amekuwa akishawishi kufanyika kwa miradi mikubwa pamoja na kampeni zenye tija kwa wilaya yake. Amekuwa mkuu wa wilaya wa aina yake, mwenye jina kubwa analolitumia kuwanufaisha watu wa wilaya yake.

Ukuu wa Wilaya haujampa Jokate kiburi, ameendelea kuwa mtu wa watu akiwaalika watu mbalimbali kumtembelea na yeye akiwatembelea watu katika maeneo mbalimbali. Wakati mwingine, huweka gari pembeni na kutembea kwa miguu.


Jerry Muro
Orodha ya wateule wa Rais Magufuli ya Julai 28 iliyowataja wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na makatibu tawala, iliendelea kuwaacha wengi na mshangao, baada ya kumtaja Jerry Muro kuwa mteule wa nafasi ya Ukuu wa Wilaya ya Arumeru.

Uteuzi wa Muro ambaye alikuwa Msemaji machachari wa klabu ya Yanga, ulikuwa gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii. Muro alikuwa anafahamika kwa utendaji kazi wa aina yake ambao haukuwa unawaacha salama wasiompenda.

Akiwa mwandishi wa habari, anakumbukwa zaidi kwa kipindi chake cha ‘Usiku wa Habari’ kupitia TBC1 kilichowanasa kwenye kamera askari wa usalama barabarani waliokuwa wanapokea rushwa.

Hata hivyo, aliachana na kipindi hicho baada ya kukabiliwa na kesi ya kuomba rushwa na kukutwa na silaha pamoja na pingu. Muro alishinda kesi hiyo, lakini hakurejea kwenye kipindi hicho, badala yake aliibukia katika Klabu ya Yanga akiwa msemaji aliyeweza kupambana vita ya maneno na mtani wake wa Jadi, msemaji wa Klabu ya Simba, Haji Manara.

Akiwa Mkuu wa Wilaya, mwaka huu wengi wanakumbuka alivyozua gumzo baada ya kuchana hotuba aliyokuwa ameandaliwa akieleza kuwa kilichoandikwa kilikuwa upuuzi.


Kadhalika, alitawala vichwa vya habari kwa namna alivyojaribu kumdhibiti yeye mwenyewe mwananchi mmoja aliyeonesha dharau wakati anazungumza, akisema “labda aje Rais’.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Arumeru, alitawala pia vichwa vya habari Septemba 5, baada ya kushindwa kujizuia na kumpa ‘makavu’ Mkurugenzi wa Wilaya aliyechelewa dakika 10 kufika eneo la tukio, mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Muro ni mmoja kati ya wakuu wa wilaya wachapakazi na ambao hawataki kucheleweshwa, hana simile na hang’ati maneno anapoona mambo hayaendi sawa. Ndivyo alivyofanya mwaka 2018.



Paul Makonda
Orodha hii haiwezi kukamilika bila kumtaja Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. Huyu sio tu kwamba alikiki mwaka huu, bali alitikisa mwaka huu kwa matukio mengi kama ilivyokuwa kwa mwaka jana. Lakini wakati huu kulikuwa na moja zito na la aina yake.

Oktoba 31, Makonda alitikisa baada ya kutangaza oparesheni dhidi ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja (mashoga) kwenye mkoa huo. Aliunda kamati ya watu 17 na alitoa namba za simu ili watu hao waweze kuripotiwa na kuchukuliwa hatua stahiki.

Zoezi hili halikwenda vizuri sana baada ya kuibuka mambo mengi na hata kuyavuta masikio ya nchi za magharibi ikiwa ni pamoja na Umoja wa Ulaya. Kampeni hii ya Makonda iliwafanya wafadhili kuitafsiri kuwa ni uvunjifu wa haki za binadamu.

Umoja wa Ulaya ulimtaka balozi wake nchini, Roeland Van de Geer kurejea nchini Brussels kwa kile walichoeleza kuwa ni kujadili hali ya kinachoendelea nchini.

Novemba 4, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kueleza kuwa kampeni aliyoianzisha Makonda sio msimamo wa Serikali.

Aidha, huu ulikuwa mwaka wa neema kuu kwa Makonda baada ya kupata mtoto wa kiume Katikati ya Mwezi Julai, mtoto aliyempa jina la Keagan. Taarifa ya kupata mtoto wake wa kwanza ilikuwa maarufu zaidi katika kipindi hicho. Kwa Makonda, hatausahau mwaka huu ambao licha ya misukosuko na changamoto za kukosolewa na kupongezwa, Keagan ni baraka isiyo kifani kwake.