NEWS

1 Januari 2019

Mwanamke Avamiwa na Simba na Kung'atwa Kalio Moja

Mkazi wa Kijiji cha Kata ya Ngwala, wilayani Songwe, Susan James, amenusurika kufa baada ya kuvamiwa na simba na kutafunwa kalio lake la kushoto wakati akimpeleka mtoto wake hospitali.
 
Diwani wa kata hiyo, Donald Maganga, alithibitisha mwanamke huyo kunusurika kifo baada ya kuvamiwa na simba huyo.

Alisema baada ya simba huyo kumjeruhi mwanamke huyo, aliondoka na kuwaacha mama huyo na mtoto wake na kwamba ni kitendo cha kumshukuru Mungu kwa kuwa mnyama huyo anapomvamia mtu anakula kila kitu na kubakiza kichwa na viganja vya mikono.

Alisema, wananchi kwa kushirikiana walimchukua mama huyo na kumpeleka zahanati ya kijiji ambako alipatiwa matibabu na baadaye walimpeleka hospitali teule ya Mwambani, iliyopo makao makuu ya wilaya kilometa 120 kutoka kwenye kata hiyo.

Alisema mbali na tukio hilo, pia kulikuwapo na tukio la mke na mume wakiwa na mtoto wao kuvamiwa na simba ambaye alimtafuna mtoto wao na wao kunusurika.

Alisema kupitia tukio hilo, anatoa rai kwa wananchi hasa wageni wanaoingia kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kufanya shughuli za kilimo kuwa makini na wanyama waliopo mbugani.

Aliwaomba watu wa maliasili kuwa waangalifu kwa kuwanusuru wananchi wanaoishi karibu na mbuga hiyo kuwaepusha na majanga ya kuvamiwa na wanyama.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mwambani, Dk. Kusenge Benangode, alithibitisha kumpokea mwanamke huyo ambaye amepatiwa matibabu na hali yake ikiendelea vizuri.