NEWS

3 Aprili 2019

Jumla Ya Tsh.bilioni 10 Zimetumika Katika Ujenzi Wa Mabweni Mapya Udsm[magufuli Hostel]

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha, amelihakikishia Bunge kuwa ujenzi wa mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yajulikanayo kama hosteli za Dk. John Magufuli uligharimiwa na serikali kwa Sh. bilioni 10.

Ole Nasha aliliambia Bunge jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Susan Lyimo, aliyetaka kujua ni kiasi gani kilitumika kujenga mabweni hayo.

Akijibu swali hilo, Ole Nasha, alisema mradi wa ujenzi wa mabweni hayo ulianza rasmi Julai mosi, 2016 na mabweni hayo yalikamilika na kukabidhiwa rasmi Aprili 15, 2017.

"Ujenzi huo ulifanywa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kama mkandarasi na kusimamiwa na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa," alisema.

Katika swali lake la nyongeza, mbunge huyo alisema gharama hiyo iliibua mjadala na waliomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), afanye ukaguzi.

"Ni jengo gani la ghorofa nne linaweza kugharimu milioni 500 tu, nilitaka kujua baada ya miezi minne yalikuwa na nyufa nyingi, lakini nyufa zilianzia kwenye msingi hadi kwenye madirisha, ni kwanini yalikuwa na nyufa hizo," alihoji. Aidha, alihoji ni gharama kiasi gani imetumika.

Akijibu maswali hayo, Ole Nasha alisema, mkandarasi aliyejenga alifanya marekebisho ya nyufa hizo na hakuna fedha za ziada zilizotolewa.

"Nimhakikishie jengo limegharimu Sh. bilioni 10, sasa kama yeye anapingana na huu ukweli niliomweleza alete gharama zake, kwa kuwa hizi ni fedha za umma na zimetumika kwa utaratibu, hakuna fedha nyingine iliyotumika zaidi ya hizo," alisema.