NEWS

2 Aprili 2019

Ommy Dimpoz: Nilimpa Kazi Lavalava Mombasa

MSANII wa Bongo Fleva, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’, amefunguka kuwa katika maisha yake haamini roho mbaya wala suala la kumbania mwenzake riziki kwani kila mtu ana yake, ndiyo maana hivi karibuni alimpatia shoo ya harusi, msanii kutoka Wasafi Classic Baby ‘WCB’, Lavalava.

Dimpoz aliyasema hayo mapema jana alipokuwa akihojiwa kwenye kipindi cha Mwendokasi kinachorushwa kupitia kituo cha mtandaoni kinachobamba hivi sasa cha +255 Global Radio, Sinza Mori jijini Dar.

Akizungumza kwenye mahojiano hayo na mtangazaji wa kipindi hicho, Mwijaku, Dimpoz alisema kuwa anashangaa sana kuona watu wakimuuliza aliwezaje kumpatia shoo ya Mombasa Lavalava wakati hawana uhusiano mzuri na uongozi wake wa WCB.

“Kiwastani katika maisha yangu siku zote huwa sina roho ya kusema nimbanie mwenzangu kupata kitu kwani hata kama tungekuwa na ugomvi kiasi gani, pale ninapoona mtu ana uhitaji, kumsaidia huwa sina kinyongo kwani naamini riziki ya mtu ipo popote.

 

“Kuna uwezekano kabisa ukaletewa dili kama ile ya Lavalava ukaibania lakini kama ni riziki yake basi ataipata tu kupitia mlango mwingine, hivyo ukiwa umembania lazima ukiona anapata, anafanikiwa basi huwa rahisi sana kujikuta ukiishia kuumia roho tu kwa ulichomfanyia mara ya kwanza.

“Hivyo watu watambue tu kuwa kwangu mimi kutoa dili kwa msanii mwingine sijaanzia kwa Lavalava kwani hata Yamoto Bendi nilishawahi kuwapa dili la shoo jijini Muscat (Oman) huku nikijua kabisa kuwa wanasimamiwa na Said Fella, hivyo mimi sijaumbwa kumbania mtu,” alisema Dimpoz

The post Ommy Dimpoz: Nilimpa Kazi Lavalava Mombasa appeared first on Global Publishers.