NEWS

4 Aprili 2019

RADI YAPENYA CHUMBANI, YAUA MAMA NA MWANAYE, WATU 6 HOI

NI simanzi kuu! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia familia ya Mbwana Said, mkazi wa Kimanzichana wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani kukumbwa na balaa kubwa. 

 

Ilikuwa Jumamosi iliyopita ambapo radi ilipenya chumbani ndani ya nyumba ya Mbwana kisha kumuua mkewe, Hadija Mikidadi (23) na mwanaye, Salima Mbwana (6) katika mazingira ambayo yaliacha mshtuko mkubwa kwa jamii.

 

Akilisimulia UWAZI tukio hilo kwa masikitiko makubwa, Mbwana alisema wakati tukio hilo likitokea yeye alikuwa njiani kurudi nyumbani akitokea Mkamba na alipofika nyumbani kwake ndipo akakutana na tukio hilo.

 

“Simu yangu ilikuwa imekorofisha kidogo hivyo sikuwa na mawasiliano yeyote. Nilipofika tu nyumbani kwangu nilishtuka kukuta watu wamejazana na muda huo tayari Polisi walishafika. “Nilishtuka sana na nilipotaka kujua kinachoendelea, nilimuona mke wangu na mwanangu wakiwa wamelazwa ukumbini huku wakiwa wameungua mno.

 

“Nilijaribu kuwaangalia vizuri ili kutaka kuthibitisha kilichotokea, lakini niliambiwa tayari wameshafariki dunia kwa kupigwa radi. “Wakati nikishangaa ndipo nikawaona wasamaria wema wakiwa wamembeba mpangaji mwenzangu, mama Husna (Mwanahija Omary) na mwanaye ambao walionekana kupoteza fahamu.

“Sikuwa na la kufanya kwa kuwa ndugu zangu walikuwa wameshafika kabla yangu. jamii. “Tulipanga na kumzika mwanangu Kimanzichana (Mkuranga) siku hiyohiyo ya tukio na mama yake naye ndiyo tukamzika juzi (Jumapili) hapa Mkerezange ambapo ndipo kijijini kwao alipozaliwa,” alisimulia Mbwana kwa uchungu.

 

Baada ya kuzungumza na mume wa marehemu, UWAZI lilizungumza na Mwanahija ambaye naye alijeruhiwa na kukimbizwa Hospitali ya Mishieni ya Kilimahewa-Kimanzichana ambaye alikuwa na haya ya kusema juu ya tukio hilo;

 

“Ninachokumbuka nilikuwa chumbani kwangu ninafanya kazi ndogondogo huku mvua ikinyesha lakini ghafla nilisikia nimepigwa shoti ya ajabu ambayo ilinirusha kutoka eneo kwenye korido karibu na chumbani kwangu hadi chumba cha watoto.

 

“Baada ya hapo sikujua kilichoendelea hadi nilipozinduka hospitalini na kumuona mwanangu naye amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake.

 

“Nilichanganyikiwa baada ya kupata taarifa za kifo cha mpangaji mwenzangu, mama Salima (Hadija Mikidadi) na mwanaye.” UWAZI pia lilizungumza na Diwani wa Kata ya Kimanzichana, Ally Ndipitipi ambaye alithibitisha tukio hilo kutokea kwenye eneo lake na kusema;

“Muda mfupi kabla ya tukio hilo ilinyesha mvua kubwa iliyoendana na muungurumo mkali wa radi ambayo wengine tulilazimika kuzima simu zetu kuhofia hali hiyo. “Baada ya mvua kutulia, mimi niliwasha simu ndipo nikapokea taarifa ya radi kusababisha maafa. Nilikimbilia eneo la tukio (nyumbani kwa Mbwana) kwa ajili ya kushirikiana na waliokuwa mahali hapo.

 

“Nilipofika nilimkuta mwanamke na mwanaye waliofariki dunia wakiwa wamelazwa chini walikuwa bado wanaungua muda huo huku wasamaria wema wakihangaika kuzima moto, lakini hata hivyo, alikuwa wameshaungua sana hivyo waliaga dunia.”

 

Diwani huyo aliwataja wengine wanaoendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Kilimahewa kuwa ni Semeni Kinjumbi na Rehema Said huku Najma Katundu akiwa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga ambaye hali yake ilielezwa kuwa mbaya akilinganishwa na wenzake.

Rais MAGUFULI Akiendelea na ZIARA Yake Mkoani MTWARA

The post RADI YAPENYA CHUMBANI, YAUA MAMA NA MWANAYE, WATU 6 HOI appeared first on Global Publishers.