NEWS

23 Novemba 2019

Bombardier ya Tanzania yakamatwa Nchini Canada

Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema ndege aina ya Bombardier Q400 imakamatwa nchini Canada.

Amesema aliyesababisha Bombardier kukamatwa ni Hermanus Steyn, raia wa Afrika Kusini ambaye alifungua kesi ya madai Mahakama Kuu nchini Afrika Kusini akidai fidia ya dola 33 Milioni.

Kesi hiyo ilisababisha Mahakama hiyo kuizuia ndege ya Tanzania aina ya  Airbus A220-300 kuondoka nchini humo Agosti, 2019.

Steyn, anadai fidia baada ya mali zake kutaifishwa na Serikali ya Tanzania mwaka 1980. Hata hivyo, Septemba 3, 2019 mahakama hiyo iliamuru ndege hiyo iliyokuwa imezuiwa katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo kuachiwa baada ya Serikali kushinda kesi bila kutoa fedha yoyote.

Akizungumza leo Jumamosi Novemba 23, 2019 Jijini Dodoma katika hafla ya kuapishwa kwa mabalozi, Profesa Kabudi amesema, “ndege imekamatwa na kesi ipo mahakamani. Aliyesababisha ni yuleyule (Steyn) aliyesababisha ndege yetu kuzuiwa Afrika Kusini.”