NEWS

9 Novemba 2019

Chama cha ACT-wazalendo chasusia uchaguzi serikali za mitaa Tanzania


Chama kingine cha upinzani chenye ushawishi nchini Tanzania kimejitoa kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa wa nchi hiyo.

Wamejitoa katika Uchaguzi huo unaotarajiwa kufanywa 24 Novemba 2019.

''Takribani, wananchi 173,593. Hata hivyo, kati ya wagombea wetu hao 173,593 waliochukua na kurejesha fomu za uteuzi, 166,649 walienguliwa katika mchakato wa Uchaguzi nchi nzima kwa sababu mbalimbali za kipuuzi na zisizo na mashiko kabisa kama ilivyoelezwa na Viongozi wetu katika nyakati mbalimbali za mchakato huu. Wanachama wa ACT waliobakizwa kwenye Uchaguzi mpaka saa Sita kamili mchana leo ni 6,944 tu sawa na 4% ya wagombea wote tulioweka.'' Anasema Zitto Kabwe kiongozi wa chama cha ACT wazalendo katika mkutano na waandishi wa habari.
Kamati ya Uongozi ya Chama Taifa ilikutana hii leo kujadili hali na mwenendo wa uchaguzi huo nchini Tanzania.

Lakini pia chama hiko kimedai kutumika vibaya kwa jeshi la polisi la nchini Tanzania kuingia mchakato wa uchaguzi huo.

''Kumekuwepo na vitendo viovu vinavyofanywa na Jeshi la Polisi na watendaji wa Serikali kuwabughudhi Wagombea wetu, wanachama na viongozi wetu maeneo mbalimbali nchini. Serikali ya Rais Magufuli isitufikishe kuvuka mstari wa Uvumilivu.'' Anaongeza Zitto Kabwe katika taarifa yake.

Mapema leo, Mbunge huyo Kigoma Mjini na kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo aliandika katika aliandika katika ukurasa wake wa twitter kuomba ushauri kwa umma kuwa wachukue hatua gani? katika mchakato unaondelea wa serikali za mtaa?